WAPARE NA UPARE "Je waijua asili ya wapare...???"
NA
Ramadhani Gidioni.
Tanzania ni nchi yenye
makabila zaidi ya 120 lakini katika makala hii nitachambua kabila la wapare, je
wapare ni kina nani? Asili yao ni nini?
Wanaishi wapi? Wanajishughulisha na nini? Lakini pia ni zipi mila na desturi
zao?
Kabila la wapare
linapatikana mkoani Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania katika wilaya ya Same na
Mwanga japo wapo wapare wanaoishi maeneo ya Moshi kama vile
chekereni,himo,uchira, mabungo na moshi mjini, vilevile wilayani Hai kwenye maeneo kama Rundugai na
mto weruweru.Mkoani Tanga wapare wanaishi zaidi lushoto katika maeneo ya
Bumbuli na Mavumo.
Asili ya wapare
inasemekana ni Taveta nchini Kenya ambako waliishi huko zaidi ya karne moja na
nusu iliyopita wakijulikana kwa jina la “waasu” wakitumia lugha iliyojulikana
kama “chasu” kabla ya kuingia Tanganyika kupitia mpaka wa Taveta.Historia
inaeleza kuwa wapare wa mwanzo walifikia katika miteremko ya mlima kilmanjaro wakiongozwa
na machifu wao mashuhuri kama vile mfumwa (chief) Boazi Mashambo ambako waligombana na wenyeji
waliowakuta maeneo hayo ambao ni wachaga waliowafukuza kutoka katika aridhi yao
hatimaye walihamia milima ya Same na Mwanga ambayo saivi inafahamika kama
milima ya upare.
Wapare wamegawanyika
katika makundi mawili wapo wapare wa kaskazini maarufu kama “vampare va mpare
ya ughu” kwa lugha ya kipare wakimaanisha wapare wa upande juu hawa huishi
wilayani Mwanga kwenye meneo ya ugweno ambao huongea lugha ijulikanayo kama
“kigweno” na wapo wanaishi maeneo ya Usangi hawa hutumia lugha ya kipare. Kundi
la pili ni wapare wa kusini “vampare va mpare ya kusea”,wakimaanisha wapare wa
upande wa chini hawa huishi wilayani Same huzungumza kipare jopo kinatofutiana
matamshi (lafudhi) na wapare wa usangi.
Kabila hili hujihusisha
zaidi na kilimo cha mahindi,maharagwe, mpunga, na vitunguu hasa kwenye mabonde
maarufu yaliyojaliwa maji na rutuba kama vile bonde la Ruvu,kisiwani, maore na
Ndungu wilayani Same vilevile maeneo ya Ugweno na Usangi wilayani Mwanga ambapo
kilimo cha migomba kimeshamiri zaidi.Same milimani pia kwenye maeneo ya Mbaga,vudee,chome
na Gonja kilimo cha migomba na nafaka kama maharagwe na mahindi hutegemewa
zaidi kama zao la chakula katika maisha ya kila siku.Katika eneo la mamba
miamba na Kanza husifika zaidi kwa kilimo cha tangawizi pia yapo mabwawa na
madimbwi mbalimbli yatumikayo katika shughuli za uvuvi kama vile bwawa la
nyumba ya mungu, bwawa la ndungu na dimbwi la msangeni.
Vile vile wapare wa
mwanzo walijihusisha na shughuli za uwindaji hasa waliokua wakiishi maeneo ya
tambarare kama vile Igoma,Njiro, Maore, Kisiwani, Mpirani ,Ndungu pamoja na
maeneo mengine wakati wapare wamilimani walijikita zaidi katika shughuli za
kilimo pia zipo koo za kipare zilizojishughulisha na ufuaji wa chuma tangu
karne ya 18, ukoo uliojikita zaidi na
shughuli hizo ni Washana waliozalisha vifaa mbalimbali vya chuma kama vile
majembe,mashoka, visu, mishale na mapanga vilivyo tumika katika biashara na
makabila ya jirani kama vile wachaga na wasambaa.
Mbali na uwepo wa
aridhi nzuri yenye rutuba kwa kilimo
katika milima na mabonde ya upare pia vipo vivutio vya utalii wa asili katika
maeneo hayo ikiwemo mito maarufu kama vile Hingilili,Rika,Nakombo, Mhoke vuta,
Yongoma, Mwetanano pamoja na maporomoko yanayosemekana kuwa marefu kuliko ya
ziwa Victoria maarufu kama “Ndurumo” yapatikanayo
eneo la Gonja bombo.
Pia ipo misitu mikubwa
ya asili kama vile Shengena ambao unasemekana ni msitu wa pili kuleta hali ya
hewa nzuri duniani baada ya Amazon,msitu wa Ngagheni Mpinji unaopatikana vudee
unaoaminika kutumiwa katika mila za kipare na matambiko kati ya karne ya 17 na
19.
msitu wa shengena.
Lakini pia upo msitu wa Wambughu uliopo karibu na kijiji cha Dangaseta
amboko moja ya koo za kipare kwa jina Wambughu ambao wengi huishi Lushoto mkoani Tanga hutambika katika moja ya muembe uliopo
ndani ya msitu huo, hata hivyo upo msitu na chanzo cha maji ya Kwachengo ambayo
ni maji ya ajabu yanayotiririka kutoka chini kwenda juu.
I
image/ndungu.com
Hali kadhalika upareni
kuna hifadhi kubwa ya Taifa inayojulikana kama Mkomazi,Bwawa la Kalimawe na
Nyumba ya mungu,milima ya Kindoroko,mokanda
na Masheko vudee ndolwa.Pia kuna majabali makubwa yavutiayo wataalii
kuja kutizama kama lile la Malameni linalopatikana Mbaga Manka ambalo zamani inasemekana
zilikua zikisikika sauti za wasichana watatu ndani ya jiwe hilo zikizungumza,
hata hivyo kuna jabali la Mhewe linalopatikana vudee ndolwa,jiwe la mkumba
vana,Ikamba, Mfinga na Lubegho linalopatikana Usangi.
Mzee eliapendavyo Elisa Mruth ni miongoni mwa wazee wa kipare
wanaoifahamu vyema historia ya kabila la wapare ambako alisema kuwa mila na
desturi za wapare zinasisitiza mafundisho mema miongoni mwa vizazi vyote kwani
wapare ni kabila lenye historia ya kupenda haki,heshima, upendo na amani katika
jamii.Alisema zamani vijana wa kipare walipofikia umri wa kubalehe walipewa
mafundisho maalumu ya kimila yaliyojuikana kama “maluthumo” ambapo vijana wa kiume walitenganishwa na
wakike katika misitu maalim iliyojulikana kama “mshitu wa mtatho” wakimaanisha
msitu wa ibada, wavulana walipewa mafundisho yajulikanayo kama “ngathu ya
mshitu” na wasichana walifundishwa katika mafunzo ya yaliyojulikana kama
“kieko” walipofundishwa jinsi ya kutengeneza familia bora na kuheshimu wazazi
na jamii nzima.
Wanawake walipojifungua
walipongezwa kwa sherehe maalum zilizoitwa “mchumbi” ambazo waliletewa zawadi
mbalimbali na wanawake wenzao katika vikapu vilivyofungwa na vitambaa kama
kaniki.Zawadi hizo mara nyingi zilikuwa asali,ndizi zilizokaushwa
zilizojulikana kama “makafi”,maziwa,mahindi pamoja na mihogo ya kukausha.Sherehe
hizi za wanawake zinafanyika mpaka leo katika kaika mila za wapare ambapo
zawadi kama sukari,mahindi,maharagwe na mafuta ya kupikia hupendelewa zaidi kwa
sasa.
Vijana wa kipare pia
waliweza kuyatunza mazingira yanayowazunguka kutokana na mafundisho na misemo
iliyojaa hekima waliopewa na wazee katika koo zao kwa mfano walifundishwa
kutunza vyanzo vya maji wakiamini misemo ya wazee wao waliowaita “vakaka”
waliosema kuwa wakijisaidia kwenye maji maziwa (matiti) ya mama zao yatakatika.
Misemo ya wazee
iliwasaidia kuwa na nidhamu,upendo na mshikamano ,maneno kama “chambi ni
kuonjanya” yakiwa na maana umoja ni mshikamano yaliwapa ujasiri wakufanya kazi
kwa pamoja na kwa upendo.
Aidha mzee Mruth
amesema kuwa mwanzoni kabla ya ujio wa waarabu na wamishenari amboko dini za
uislamu na ukristo zilikua hazijafika katika jamii za wapare watoto walipewa
majina kutokana na matukio maalumu wakati mototo wanapozaliwa mfano mototo wa
kiume aliyezaliwa wakati wa vita aliitwa Senkondo wakati wakike aliitwa
Nankondo,mathalalani watoto waliozaliwa wakati wa mvua waliitwa “Nambua” wakati
wakati wa usiku waliitwa “nakio” na hata waliozaliwa wa wakati wa shida kama
vile njaa waliitwa majina yanayoshabihiana na wakati huo mfano “Senzota”, nzota
ikiwa na maana ya njaa.
Pia majina ya maeneo
mbalimbali yalitokana na majina ya koo za kipare zinazoishi maeneo hayo mfano
maeneo kama Chome wanaishi ukoo wa
wachome,Gonja wanaishi wagonja, Mbaga wanaishi wambaga,ugweno wanaishi wagweno
na maeneo mengine mingi yalipewa majina kwa misingi hiyo.
Hata hivyo mila na
desturi za wapare zimebadilika sana katika miaka ya hivi karibuni kutokana na mabadiliko ya sayansi na
teknolojia,maendeleo ya utandawazi, elimu ya magharibi pamoja na mafunzo ya
dini yaliyobadilisha imani za watu katika kabila hilo hali iliyopekea kuacha
kabisa ibada zao na mitambiko katika misitu mikubwa na majabali na kujikuta
wakifwata maandiko ya msaafu na bibilia ya kuabudu mungu katika makanisa na
misikiti.
Na
Ramadhani Gidion.
UDSM-SJMC
No comments
+255716829257