Habari mpya

Wakili wa Hifadhi ya Wanyama Arusha, Maneno Mbunda atoweka kwa siku 7 sasa

Mwanasheria wa Hifadhi ya Wanyama Arusha (Arusha National Park), Wakili Maneno Mbunda amepotea katika mazingira ya kutatanisha kwa siku 7 sasa (tangu Aprili 28 mwa huu).
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeeleza kuwa Wakili Maneno Mbunda alikamatwa na watu waliosadikiwa kuwa ni askari wasio na sare za kiaskari na kisha kuelekea kusikojulikana.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa rafiki wa karibu wa wakili huyo, magari yaliyotumika kumkamatia wakili huyo hayakuwa na namba za usajili.
Imeelezwa kuwa Wakili huyo alikamatiwa eneo la Usa River jijini Arusha na hajulikani alipo mpaka sasa, na hakuna anayejua sababu za kutoweka kwake.
Juhudi za kumtafuta Wakili Maneno zilianza tangu Jumapili ambapo ndugu na mke wake walizunguka vituo kadhaa vya polisi mkoani Arusha lakini hawakuweza kumpata.
THRDC imesema kuwa, kwa mujibu wa sheria za nchi, hata kama wakili anasadikika kuna kosa ametenda bado utaratibu wa kisheria ungepaswa kutumika kumkamata na kumpeleka katika vyombo vinavyotambulika kisheria.
Utaratibu huu umeleta taharuki na hofu kubwa kwa familia kwani hakuna mwenye uhakika kamili ndugu yao yupo wapi.
Hadi jana Mei 3, 2019 mke wa wakili huyo hakuwa ameweza kufungua kesi ya kutoweka kwa mume wake katika Kituo cha Polisi Usa River, kutokana na mkuu waupepelezi wa kituo hicho hayupo ofisini.
Tukio la kupotea kwa Maneno limeibua tena mijadala kuhusu kupotea kwa
Wakili wa Kujitegemea Philbert Gwagilo aliyepotea miaka minne iliyopita, na hadi leo hafahamika alipo.
Tunavisihi vyombo vya usalama hasa Jeshi la polisi mkoani Arusha kufanya uchunguzi kwa uharaka ili kuweza kupatikana kwa wakili Mbunda, THRDC imeeleza katika tamko lake.
Pia mtandao huo umemtaka mwajiri wa Wakili Mbunda achukulie suala hilo kwa umuhimu mkubwa na kutoa ushirikiano kwa familia ya Wakili Maneno Mbunda pamoja na Jeshi la Polisi ili kusaidia uchunguzi wa kutoweka kwa wakili kwake.

No comments

+255716829257