JE UPENDO WA DHATI PEKEE NI NGUZO YA MAHUSIANO??
Ukisoma kwa kutafakari makala hii utagundua kuwa kuweza kujifahamu
sisi wenyewe vema, kuweza kujitawala sisi wenyewe, na pia kuweza ‘kuwasoma’
vema wenzi wetu , ni mambo ya msingi sana ili upendo tulionao uweze kudumisha
mahusiano. Msisitizo ni kwamba, pamoja na ukweli kuwa upendo ni kitu cha
muhimu katika mahusiano, makala hii inaeleza kuwa kutegemea upendo pekee kama nguzo kuu ya mahusiano bora kunaweza kuwa jambo la hatari kwa
mahusiano, kwa sababu zipi?
1. Binadamu ni kiumbe huru: Ni muhimu kukumbuka hili hasa kama unadhani kwakuwa unampenda
fulani na umemuonyesha mapenzi yako yote basi hicho ni kama kifungo kwake kuwa
hatoweza kutoka katika penzi lenu. Kwa asili binadamu ni huru, na anaweza
kuamua kuutumia uhuru wake kufanya maamuzi mengine yoyote tofauti na
unavyofikiri ni lazima afanye. Kwa kuwa pia ni mbinafsi, basi
kama upendo wako wote kwake hauendani na yale anayotazamia , unaweza kukuta
ameshindwa kukaa katika penzi , ambalo kwa watu wengi wanaona kuwa ni penzi
zito.
2. Binadamu ni mbinafsi kwa
asili: Binadamu kwa asili huangalia maslahi yake kwanza kabla ya
kuangalia ya mwingine. Mfano dhahiri wa ubinafsi huu ni pale inapotokea ajali ,
mara nyingi mtu huwaza kujiokoa mwenyewe kwanza kabla ya kufikiria wa karibu
yake. Tumesikia habari za mama mzazi kuacha kitoto kichanga ndani wakati moto
ukiendelea na yeye kutoka nje. Kuna habari pia za mama kumtumia mtoto wake kama
‘kifaa’ cha kuvunjia kioo cha gari , ili aweze kujiokoa, pale ambapo ajali
ilitokea. Hivyo upendo tuu pekee hautoshi kumfanya mtu aendelee kukaa katika
ndoa au mahusiano kabla ya ndoa (uchumba), ni muhimu yawepo mambo mengine yenye
manufaa kwa mtu husika.
3. Binadamu ana mahitaji
mengi na yasiyo na kikomo: Mwenza wako ana mahitaji
mengi na yanaongezeka na kubadilika siku hadi siku kutegemeana na mabadiliko
mbalimbali kama vile hali ya hewa, aina ya kazi, watu anaokutana nao, mabadiliko ya teknolojia, mabadiliko ya
kiuchumi n.k. Upendo wenu, hausimamishi mahitaji haya yasitokee, na kwamba
upendo pekee hauwezi kuwa jibu la kutimiza mahitaji hayo. Inahitajika bidii
katika kujituma kujiletea kipato, kuwa na mawasiliano bora kati yenu, kutambua
mabadiliko na kuchukua hatua kabla mabadiliko hayajawabidilisha, na zaidi sana
muweze kuwa na utamaduni wa kupanga mambo pamoja na kuwa waaminifu katika
kutimiza yale mnayopanga.
Chukulia mfano, wa wanandoa
walioishi vema kwa miaka 5 ya ndoa, halafu ndoa ikaanza kulemaa kwa kuwa mmoja
wao anaona hakuna uwajibikaji katika kumsaidia mwengine kujiendeleza kielimu,
kibiashara, au kutimiza ndoto nyingine ambayo mwanandoa amekuwa nayo.
4. Binadamu wengi wanashindwa
kujitawala: Uwezo wa mtu kujitawala unaweza ukakinzana na upendo wake
kwa mwenza wake, hivyo kuleta hali ya kutoridhika kwa mwenzi wake, kitu ambacho
kinapunguza au pengine hata kuondoa raha ya
mahusiano.
Mfano utakuta kwa kufuata
makundi ya marafiki aliyonayo, mwanaume anakuwa mlevi wa kupindukia, na kujikuta akiingia katika anasa na maamuzi mengine yasiyo mazuri
kwa mpenzi wake na familia kwa ujumla. Hata hivyo mwanaume huyo huyo ukimuuliza
kama anampenda mke wake au la, atakujibu anampenda sana. Tatizo nini ?
Utajibiwa, ni pombe tuu ndio mmemtawala, na kwamba jamaa ana ‘kampani’ mbaya.
5. Maana isiyo sahihi ya
upendo: Kuna wengi wanaodai wanao
upendo lakini kiukweli walichonacho sio upendo bali ni tamaa au matakwa ya
kuhitaji kutimiziwa mambo fulani.
Maana halisi ya upendo sio vile
unavyotaka fulani akufanyie mambo au jambo fulani, upendo sio vile unavyojisikia
baada ya fulani kukutendea jambo uliloliona jema kwako, upendo sio vile fulani
anavyokufanya ujisikie kwa sababu ya sura yake au umbo lake, BALI, upendo ni
utayari wako wewe kufanya mambo yanayompendeza mwingine, kuwa tayari kuona
mwingine ana furaha juu yako.
Kwa maana rahisi , upendo
si jambo linalokuhusu wewe unajisikiaje, bali ni vile unavyotaka mwingine
ajisikie.
Kwa maana nyingine, utatimiza
vema upendo wako kwa kujitahidi kumfahamu mwenza wako, kutimiza yale
anayohitaji (ili awe na furaha) sio kutimiza yale unayotaka wewe kwa makusudio
yako binafsi. Upendo unahitaji kumheshimu mwenza wako, kumsikiliza, kumfanya
akuamini, na aendelee kukuamini.
Pamoja na kuwa hisia za kimwili
(chemistry) ni muhimu sana katika kujenga mahusiano yenu, hisia za kimwili zisichanganywe na upendo.
Kwakuwa fulani amekuvutia
kimwili haina maana kuwa basi unampenda mtu huyo.
Kufanya tendo la ndoa, sio
lazima iwe ndio ishara ya uwepo wa upendo katika yenu, kwani wapo hata
wanaofanya tendo la ndoa kama biashara
No comments
+255716829257