ZIJUE ATHARI ZA MALEZI YA KIBAGUZI KWA MTOTO ASIYE WA DAMU.
Mtoto yeyote ana haki kisheria awe
ni yatima, mlemavu au anaishi mbali na wazazi wake. Ikiwa ni kuthaminiwa na
kupatiwa mahitaji yote ya msingi, kama vile elimu, matibabu, chakula bora,
kucheza, kupumzika, kutoa maoni na kuskilizwa pasipo kubaguliwa kwa namna
yoyote.
Leo tunaangalia malezi ya watoto
ambao siyo wa damu yako (yaani si wa kwako wa kuzaa), wanaweza kuwa wa ndugu
zako au la.
Yamkini unaishi nao kutokana na wao
kufiwa na wazazi, wazazi wao kutokuwa na nafasi ‘kihali’ kuwahudumia au sababu
fulani ambazo zimepelekea wewe kuwa mlezi wao. Kuna tabia zimejengeka katika
jamii juu ya malezi ya watoto wanaolelewa na walezi wa namna hii.
Watoto hawa wamekuwa wakiishi katika
mazingira magumu kwa kunyimwa haki zao za msingi, kufanyishwa kazi ngumu bila
kujali umri na uwezo wao, kutokupelekwa shule, kutukanwa matusi, kunyimwa
chakula na kadhalika kwa kigezo kuwa si watoto wa kuwazaa.
Hili hufanyika wakati walezi hawa wakiwapatia
malezi bora na mahitaji yote watoto wao wa kuwazaa! Hii ni mbegu ya kibaguzi,
ubaguzi wa ‘nafasi’ kimaisha!
Watoto hawa huamshwa majogoo kuteka
maji, kufua nguo za watu wote nyumba nzima, kuosha vyombo na kusafisha nyumba
wakati watoto wa mlezi wao wakiwa wamechapa usingizi.
Yaani mtoto anakuwa mtumwa na
akikosea kidogo hupigwa na kuumizwa hivyo kukosa raha kabisa. Watoto namna hii
hukimbilia mitaani na kuhatarisha maisha yao zaidi.
Tafiti zinaonyesha kuwa watoto wengi waishio
na kufanya kazi mitaani nchini Tanzania hutokana na malezi ya unyanyasaji
waliyoyapata kutoka kwa wazazi ama walezi wao na hivyo kukimbilia mitaani ili
kupata amani.
Pia tafiti zinzonyesha kuwa watoto
wanaolelewa namna hii hujengewa chuki yenye kudumu mioyo mwao kwa muda mrefu na
aghalabu hujenga nia ya kulipiza kisasi kwa waliowatendea vibaya au kwa watu
wengine.
Vilevile upo ushahidi wa kitaalamu
unasema kuwa watoto hawa wana uwezekano mkubwa wa kuwa wahalifu na kukosa
huruma na upendo kwa binadamu wenzao.
Hakuna mtoto ambaye anatamani kuishi
mbali na wazazi wake bali ni safari ya maisha inayowalazimu kuishi katika
familia baki.
Ukinuia kumlea mtoto wa binaadamu
mwenzio, huna budi kumlea katika usawa na kumpatia haki za msingi ikiwa ni
pamoja na mapenzi kama ufanyavyo kwa watoto wako. Hakika, tena kwa mifano
iliyopo katika jamii zetu, hawa wakifanikiwa – watakulea uzeeni.
Post Comment
No comments
+255716829257