Habari mpya

Abdallah Mtolea ahamia CCM

ALIYEKUWA Mbunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF, Abdallah Mtolea, ametangaza kujivua uanachama wa chama hicho na kujiuzulu ubunge, huku Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Magdalena Sakaya akisema mbunge huyo ndiye aliyekuwa chanzo cha mgogoro ndani ya chama hicho.
Mtolea alitangaza uamuzi huo bungeni Dodoma jana   baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kumpa nafasi ya kuchangia Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha wa Mwaka 2018.
Mtolea aliposimama alisema mwanzo aliomba kuchangia lakini anachukua fursa hiyo kutangaza kujiuzulu ubunge kwa sababu ya hali ya mgogoro ulio ndani ya CUF kati ya kundi linalomuunga mkono Katibu Mkuu wa CUF, Maalimu Seif Sharif Hamadi na wale wa Profesa Ibrahim Lipumba.
“Nimelazimika kuandika barua ya kujiuzulu ubunge wangu siyo kwa kupenda bali ni kutokana na hali ndani ya chama changu.
“Mgogoro ndani ya chama changu ndiyo ulionisukuma, mgogoro umekuwapo ndani ya miaka miwili sasa.
“Wabunge mnajua ili uweze kutimiza wajibu wako wa ubunge ni lazima utumie mtandao wa chama, lakini ndani ya chama chetu hali ni ngumu.
“Na nilishapata taarifa kwamba wakati wowote wiki ijayo nilikuwa nivuliwe uanachama wangu kwa hiyo nimeona badala ya kwenda kusubiri taarifa mbaya nyumbani bora niwahi ili niizoe. Kwa sababu ya huu mgogoro imefika mahali mpaka huko mitaani tunatishiwa maisha.
“Kwa hiyo nawashukuru wote kuanzia wewe Spika (Job Ndugai) kwa ushirikiano tuliokuwa nao hapa, Waziri Mkuu, wabunge wenzangu haswa wa kambi ya upinzania ambao mmekuwa karibu na mimi hata wale ambao hawatafurahishwa na uamuzi wangu huu.
“Najiuzulu nikiwa bado natamani kuwahudumia wananchi wa Temeke kwa hiyo nawakaribisha vyama vyote kuanzia Chadema, NCCR,  ACT na CCM kujadiliana namna tutakavyoweza kushirikiana,” alisema.
Mtolea pia alitoa shukrani kwa wanachama wote wa CUF ambao hawamuungi mkono Profesa Lipumba.
Baada ya kutoa kauli hiyo, Spika alimtaka kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.
Naye   kabla ya kutoka nje alikwenda kumpa mkono Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira Kazi na Vijana, Jenister Mhagama, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini huku Mbunge wa Tunduma,  Pascal Haonga (Chadema) akikataa kuupokea mkono wake.
Baada ya Mtolea kuzungumza, Spika wa Ndugai alisema, “Naomba niliarifu Bunge rasmi kuwa nishapata barua ya Mtolea ya kujitoa CUF.
“Taratibu za kuandikia barua kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zitafuata na mengine yataendelea, msiwe na wivu kama Haonga anayekataa kutoa mkono wa mtu aliyechukua uamuzi wake binafsi,” alisema
Akizungumza nje ya viwanja vya Bunge, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magdalena Sakaya, alisema Mtolea alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa wanachochea mgogoro ndani ya chama hicho hivyo bora alivyoamua kuondoka mwenyewe.
Alisema tayari alishapewa maonyo kadhaa lakini alikuwa hasikii na hivyo yawezekana amejua kuwa anaweza kuchukuliwa hatua za nidhamu hivyo akaamua kujiwahi.
Alisema pia mgogoro wa CUF unachochewa kwa kiasi kikubwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalimu Seif Sharfu Hamadi, ambaye amekataa kukutana na Mwenyekiti wa Chama hicho anayetambulika na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
“Maalim Seif amekataa kabisa kumaliza mgogoro ndani ya chama licha ya kufuatwa na mpaka viongozi wa dini.
“Alikubali kukaa na CCM kule Zanzibar licha ya kuwa watu waliuawa mpaka wakaandika Katiba nyingine lakini kumaliza huu mgogoro wa chama kakataa.
“Jambo hili naamini litamalizwa na mkutano mkuu wa chama ambao utakaa karibuni kwa sababu ndiyo ngazi ya juu kabisa ya chama chetu, ila niwaambie tu kuwa chama chetu kiko salama kabisa,” alisema Sakaya.
Hata hivyo, Mtolea atakumbukwa akiwa CUF akihudumu kama Naibu Mkurugenzi wa Sheria, alitangaza operesheni ya kusafisha ofisi ya CUF Buguruni kwa kudai imevamiwa na watu na wamechafua mazingira ikiwa na lengo la kumuondoa Lipumba
Mtolea amekuwa mbunge wa tatu wa CUF kujiuzulu, wa kwanza alikuwa Abadala Mtuliya wa Kinondoni, aliyehamia CCM na Zuberi Kuchauka, aliyehamia CCM.  Wote waliteuliwa tena kutetea nafasi zao na kutangazwa kuwa washindi.
Jana, wakati Mtolea akijiuzulu, wabunge wanne waliojiuzulu kutoka Chadema na kujiunga na CCM  waliapishwa kuendelea kushika nafasi zao.
Wabunge hao ambao walipita bila kupigwa, awali Spika Ndugai alitangaza kwamba walikuwa waapishwe katika mkutano wa Bunge wa Januari.
Lakini jana waliapishwa huku akiwa hajasema nini kimefanya ratiba aliyotangaza Novemba tano ibadilike.
Wabunge walioapishwa jana ni James Millya (Simanjiro), Joseph Mkundi (Ukerewe), Pauline Gekuli (Baba mjini), Ryoba Marwa (Serengeti).
KUHUSU KUHAMIA CCM
Abdallah Mtolea ametanabaisha kuwa kwa sasa ili uwawakilishe wananchi vizuri inabidi uwe CCM kwani ndo kuna sera za kusaidia wananchi kwa sasa. Hivyo imekuwa ikimuwia vigumu kufanya kazi akiwa nje ya CCM.
Mbunge huyo amesema kwa hiari yangu ameamua kujiuzulu uanachama wa CUF na kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi nilizokuwa nashikilia kuanzia Desemba 2, 2017.
Amesema s​ababu za kuchukua uamuzi huo ni kutokana na uzoefu alioupata kwa miaka miwili ya ubunge ambapo amebaini kuwa Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani na imefanya vizuri katika mambo mengi ambayo upinzani waliahidi kuyatekeleza.
Hivyo haoni sababu ya kuendelea kuwa upinzani na badala yake ameona ni vema aungane na juhudi za Serikali kwa kumuunga mkono Rais Magufuli katika kuwaletea wananchi maendeleo na kukabiliana na kero mbalimbali.

No comments

+255716829257