Habari mpya

BENKI YA EXIM YA CHINA KUTOA MKOPO WA UJENZI WA RELI YA KATI..

 
Benki ya Exim ya China imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani Bilioni 7.6 sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 16 za kitanzania kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi mkubwa wa reli ya kati hapa nchini kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) unaotarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha.

Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang amemueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Julai, 2016 kuwa pamoja na kutoa fedha hizo zitakazofanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli ya kati benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshajiwa reli.

Pamoja na kukubali kutoa fedha hizo, Rais huyo wa Benki ya Exim ya China amempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa dhamira ya dhati ya kuiletea nchi maendeleo ikiwemo kuharakisha ujenzi wa reli ya kati na ameahidi kuwa benki yake itatoa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha mradi huo na miradi mingine ya maendeleo.

''Kuhusu huu mradi wa reli ya kati tuna mtazamo chanya, tunauona ni mradi mzuri na tutatoa ushirikiano wowote utakaohitajika. Tunaamini kuwa kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania mchakato wa utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa mafanikio na kwa kuzingatia muda "Amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang kwa kukubali kutoa fedha hizo na amemuhakikishia kuwa Tanzania imedhamiria kutekeleza mradi huo ambao tayari ujenzi wake umepangwa kuanza katika mwaka huu wa fedha kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha shilingi Trilioni 1 zilizotengwa katika bajeti.

Rais Magufuli amebainisha kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi na Congo.

"Kwa hiyo kukubali kwao ambako ilikuwa ni kitu kikubwa, inaonesha kwamba juhudi za Tanzania kwenda haraka haraka zinakubalika kimataifa, na wenzetu hawa wachina wana pesa nyingi.

''Na kule kuaminika kwamba tunakopeshwa kwa masharti nafuu, riba yake ni ndogo na huku kwetu ni mafanikio makubwa, kwa hiyo mizigo mingi tutakuwa tunaisafirisha, tutaendeleza reli yetu na bandari zetu" Amesema Rais Magufuli.

Mradi wa ujenzi wa reli ya kati utahusisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es salaam-Tabora-Isaka-Mwanza, Tabora-Mpanda Kalemela,Tabora-Uvinza-Kigoma na saka-Keza-Msongati.

Mazungumzo kati ya Rais Magufuli na Rais wa benki ya Exim ya China yamehudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba.

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU Dar es salaam

20 Julai,2016
Magu CHINA.jpg

No comments

+255716829257