Trump achekwa kwa alivyotamka Tanzania
Mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump amekejeliwa mtandaoni baada ya kuonekana akiboronga akitamka Tanzania wakati wa kutoa hotuba.
Bw Trump alikuwa akizungumzia mashambulio ya kigaidi yaliyotekelezwa katika mabalozi ya Marekani nchini Kenya na Tanzania mwaka 1998 wakati wa kuzungumzia sera yake ya kigeni.
Badala ya kutamka vyema ‘Tanzania’ anasikika akitamka ‘Tan-zay-nia’.
Mashambulio hayo yalitekelezwa na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
Msemaji wa ikulu ya White House pia alimcheka Bw Trump alipoulizwa kuhusu vile mfanyabiashara huyo tajiri kutoka New York alivyotamka jina Tanzania.
“Kweli, yamkini jinsi ya kutamka huwa haijaelezwa kwenye kifaa cha kuonesha maandishi ya hotuba,” alieleza afisa wa habari wa ikulu Bw Josh Earnest.
Wakati wa hotuba hiyo, alizungumzia pia kuhusu kundi la Islamic State ambalo kwa sasa limeanza kunawiri nchini Libya. Kundi hilo hujulikana pia kama Isis.
“Na sasa Isis wanapata mamilioni na mamilioni ya dola kila wiki kwa kuuza mafuta ya Libya. Na wajua? Huwa hatuwawekei vikwazo vya kutouza, hatuwaangushiwi mabomu, hatufanyi lolote,” alisema.
“Ni kana kwamba nchi yetu haifahamu yanayofanyika, jambo ambalo huenda likawa kweli.”
Kwenye hotuba yake, Bw Trump alikosoa sera za kigeni za Rais Barack Obama.
Lakini Bw Earnest alipuuzilia mbali madai ya Bw Trump ambaye kwa sasa anaongoza miongoni mwa wagombea wanaotaka kupeperusha bendera ya chama cha Republican.
CHANZO: BBC
No comments
+255716829257