Habari mpya

Syria: Mataifa yaafikiana vita visitishwe

LavrovImage copyrightAFP
Image captionSergei Lavrov na John Kerry wamekuwa wakishiriki mazungumzo hayo mjini Munich
Mataifa yenye ushawishi duniani yameafikiana kuhusu mkataba wa kusitisha mapigano nchini Syria ambao utaanza kutekelezwa katika kipindi cha wiki moja ijayo.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mazungumzo nchini Ujerumani.
Mwafaka huo hata hivyo hautahusisha makundi ya kijiihadi ya Islamic State (IS) na al-Nusra Front.
Mawaziri wa mataifa wanachama wa Kundi la Kimataifa la Kusaidia Syria pia wamekubaliana kuharakisha na kuongeza juhudi za kutoa misaada.
Tangazo hilo limetokea huku jeshi la Syria, likisaidiwa na Urusi kwa mashambulio ya kutoka angani, likiendelea kupiga hatua eneo la Aleppo.
Hatua hiyo ya kijeshi inatishia kuzingira maelfu ya raia katika maeneo mengi ya mji wa Aleppo yanayodhibitiwa na waasi.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry amekiri kwamba mpango wa kusitisha mapigano unaazimia kutimiza makuu lakini akasema changamoto kubwa itakuwa kuona iwapo pande zote zitaheshimu mkataba huo.
Image captionWatu wengi wametoroka mapigano Syria
“Kile tulicho nacho kwa sasa ni ahadi kwenye karatasi, siku chache zijazo tunafaa kusubiri tuone iwapo hayo yatatekelezwa,” amesema.
Jopo kazi linaloongozwa na Marekani na Urusi litasaidia kutekeleza mkataba huo kupitia mashauriano na makundi yanayopigana nchini Syria.
Misaada inatarajiwa kuanza kufikishwa kwa raia waliozingirwa na majeshi katika baadhi ya maeneo Ijumaa.
Bw Kerry ametoa tangazo la kupatikana kwa mwafaka huo akiandamana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov na mjumbe maalim wa Umoja wa Mataifa Syria, Staffan de Mistura.
Bw Lavrov amesema kuna sababu za kuwa na matumaini kwamba “tumefanya kazi kubwa na nzuri leo”. Pendekezo la awali kutoka Urusi lilikusudia mapigano yasitishwe kuanzia tarehe 1 Machi.

No comments

+255716829257