Habari mpya

Uchambuzi wa album bora za zamani za bongo flava..

Image result for old bongo flava
Zamani kidogo mwishoni mwa miaka ya 90 mpaka 2009 hivi ungekuwa sio mwanamuziki uliyekamilika kama hukuwa na album sokoni! Ili uwe mmoja kati ya wasanii wakali ni lazima Album yako iliyosheeni ngoma zako kali iwe inapigwa kwa wingi kwa wale jamaa wauza kanda za wasanii wa Bongo Flava.
Nakumbuka wakati ule nilipokuwa naweka 100, 100 za shule ili nipate hela za kwenda kununua album za akina Jay Moe na Juma Nature. Maisha yanaenda kasi mno leo wakina Ommy Dimpoz wamegoma kutupa huu uhondo.
Unabaki na mshangao ukijua kuwa wasanii kama Rich Mavoko,Ommy Dimpoz wana miaka zaidi ya mitano kwenye game wakiwa hawana japo album moja kwenye makabati yetu.
Siku hizi wanashindana kwa video bora na sio album bora tena.
Mambo mengi yalitokea hapa katikati na tukasikia mengi pia yaliyokwamisha maisha yale ya kuvutia kupotea. Wanasema “wadosi” walikuwa wakipata kikubwa huku wasanii wakipata kiduchu na kupelekea kususa kutengeneza album na matokeo yake kuishia kutoka nyimbo,kufanya video kali na kusubiri mikataba ya show kila mtu kasahau kuhusu maisha ya album.
Orodha hii inakuletea album 10 bora zaidi kwenye Bongo Flava ambazo mpaka leo zimeacha historia:
Historia ya Kweli
Mwanasesere Prince Dully Sykes kwenye ubora wake. Ilikuwa mwaka 2003 album ile ilifuatana na wimbo mkali zaidi kutoka kwenye album ile na pengine ni wimbo mkali zaidi kutoka kwa Mr.Misifa,Ungethubutu kusema nini zaidi kuhusu wimbo wa Salome? Kwenye album ile ungekutana na simulizi nzuri mno tena zenye ukweli ndani yake.
Tamika msichana aliyemkimbia na kumuachia watoto, Hajisadi mshkaji wake ambaye alikufa kwenye meli baada ya kutoswa baharini, Nyambizi jimama lilionyesha mahaba kwake,Sharifa wimbo uliobeba jina la album maana ile ilikuwa ni historia ya kweli ya msichana aliyekimbia shule na kuyavagaa maisha ya mtaani kwa pupa na kuambulia Ukimwi, Julietha aliyekuwa anampenda kwa dhati bila kusikia maneno ya wanafiki ungepata pia simulizi nzuri ya Kijakazi mtoto wa kizaramo aliyeteka akili ya Dully vya kutosha.
Miika Mwamba ndiye producer aliyefanya ngoma nyingi zaidi kwenye album hii. Album zake mbili zilizofuata Handsome ya mwaka 2004 na Hunifahamu ya 2005 hazikuwa na ubora wa Historia ya kweli.
Ugali
Diamond Jubilee, watu walikula Ugali jukwaani,moja kati ya show chache zilizoweza kuujaza ule ukumbi. Toka pale wasanii wengi wamekuwa wakiukimbia ule ukumbi kwa kuogopa kutumbuiza viti ila Juma Kassim Ally Kiroboto aliweza kufanya maajabu yake kwenye ukumbi ule.
Akitoka kugombana na mpenzi wake Sinta wakati ule Juma alirudi akiwa na hasira ya mapenzi. Huwezi kubisha album ile ilibebwa na nyimbo nyingi za mapenzi zaidi tofauti kabisa na album yake ya kwanza ya Nini Chanzo iliyotoka mwaka 2001 ukiondoa wimbo wa Sonia, sidhani kama kulikuwa na wimbo mwingine wa mapenzi.
Hata album yake iliyofuata ya Ubinadamu Kazi ya mwaka 2005 haikuwa na nyimbo za mapenzi kama hii. Sitaki Demu,Ahh Wapi, Inaniuma Sana, Ugali,Rudi Nyumbani, Kisa Demu, Umoja wa Tanzania, Hali Ngumu – ni nyundo tupu za kwenye album hii ya kiistoria kwenye Bongo Flava.
Beat nzuri zote kutoka kwa P.Funk toka mwaka 2003 mpaka leo hazijawahi kupoteza ubora wake na huwezi kuwa na hofu ukisema hii ni album bora zaidi kutoka kwa “mhuni” huyu wa Temeke na bora zaidi ya album yake ya kwanza, Nini Chanzo, Zote History ya mwaka 2006 na hata Tugawane Umaskini ya mwaka 2009.
Kamanda
Daz Baba,Ferooz, Critic,La Rhumba na Sajo ni muunganiko fulani mtamu wa washkaji kutoka Azania,Jitegemee na maskani yao kule Kimara.
Walikuwa na umri mdogo mno wakati ule ila nyimbo zao za ujumbe na huzuni zingekuacha ukiwa unawakumbuka muda wote kwa uzito wa mistari yao.
Kwa bahati mbaya kwao haikufata album nyingine yoyote kutoka kwao baada ya album hii ya kihistoria. Mwisho wa siku Ferooz alikuja na album yake ya Safari huku Daz Baba akija na Elimu Dunia na wenzao wote walipotea na kundi lao.
Kamanda ni wimbo uliobeba jina la album na wimbo ulioacha watu wengi midomo wazi kwa majamaa kujichulia vifo vyao ila Barua ni wimbo uliomaliza kila kitu na kuipeleka album yao sokoni wakijidai. Nitafanya Nini,Matatizo,Maji ya Shingo Nashuka Rhymes na nyingine kali zilizoibeba album hii ya kibabe.
Mika Mwamba na P.Funk Majani ndio wapishi waliotengeneza nyimbo nyingi zaidi kwenye Santuri hii.
Ulimwengu Ndio Mama
More Tech,More Flava,Mo Skills,Mo Genius, Superman. Maisha ya boarding noma Jay Moe alisema huko ndiko alipolipata neno Ulimwengu Ndio ,Mama. Hiyo ni mistari fulani mikali kwenye wimbo huu wa maisha ya boarding kutoka kwenye album ya hii ya kishujaa.
Nyimbo kama Bishoo,Misosi Mitungi na Pamba, Ni Mshamba,Majukumu, Narudi Shule zilikuwa ni nyimbo kali mno kutoka kwenye album hii ila wimbo wa “Kama Unataka Demu” unabaki kama wimbo bora zaidi kutoka kwa Jay Moe.
Kwa wengi Jay Moe anachukuliwa kama msanii asie na bahati ila niamini mimi na rudi nyuma kidogo itafute album hii, isikilize kwa utulivu utakuja kugundua madini yalio mchangani ila watu wameshindwa kustukia. Alikuwa na ushkaji mkubwa mno na P.Funk na hivyo ni jambo jema ukijua Majani ndio aliyeipika album hii.
AKA Mimi
Albert Mangwea(rip) kutoka Dodoma na wanae wa East Zoo,Chamber Squad alikuja kuleta kitu bora zaidi kitakachoishi kwa miaka mingi mno.
Popote unaweza kwenda ila huwezi kukuta album ambayo ndani yake kila wimbo ni hit song. Kwa wasanii wengi unaweza kukuta album ina nyimbo 10 basi nyimbo kali zaweza kuwa 4 au 5 nyingine ni za kujaza album tu iende sokoni ila kwa Ngwea ilikuwa tofauti mno kuanzia wimbo wa kwanza mpaka wa mwisho, zote zilikuwa za moto, nyimbo ambazo zinaishi hata baada ya kutokuwepo kwake.
Ghetto Langu ulikuwa wimbo wa kwanza kwenye album hii. Huu ni ni wimbo uliomtoa Ngwea kutoka msanii wa kawaida tu mpaka kwenda kuwa staa anayegombaniwa kwenye show.
Mikasi ni wimbo mwingine mkubwa zaidi uliofuata kwenye album hii huku nyimbo kama Sikiliza, AKA Mimi, Zawadi,Dakika Moja, Napokea Simu, Bila Muziki,Mademu Zangu,Weekend na She Got A Gwan zinafuatana kwenye album hii iliyopikwa kiufundi na Majani. Album hii iliyotoka mwana 2003 ni album kali zaidi ya album yake Nge iliyofuata mwaka 2010.
Funga Kazi
Hii ilikuwa ni album ya mwisho ya Hard Blastaz Crew kabla ya kila mmoja kwenda na njia yake. Hapo unawazungumzia Big Willy,Terry Fanani wa kigogo na Profesa Jay.
Likiwa limetoka kubeba tuzo ya kundi bora la hip hop mwaka 1999 ndio mwaka 2000 walipokuja na album hii iliyosheeni ngoma kali tu.
Wimbo kama Chemsha Bongo ungekupa ujumbe mzuri mno, ni wimbo uliObadilisha fikra za wazee wengi kuanza kuona kuwa Bongo Flava sio uhuni na ungEpata ujumbe mwanana mno ndani yake.
Mamsap ni wimbo mwingine mkubwa kutoka kwenye album hii, Chuzi Limekubali, Nusu Peponi nusu Kuzimu na wimbo kama Ehh Mola zingekupa ujumbe mkali mno kama kawaida ya nyimbo za HBC wakati ule.
Nitakupa Nini
Amiri Jeshi Mkuu wa Upanga East Coast, Crazy GK, yupo kimya sana siku hizi ila album hii inabaki kuwa moja kati ya album bora za muda wote kwenye Bongo Flava. Sister Sister ni wimbo mkubwa mno uliokuwa ukiwaasa vijana na gonjwa hatari la ukimwi. Tutakukumbuka ni wimbo mwingine uliomuhusu “mshkaji” wake aliyefariki kwa ajali ya gari pamoja na Kosa Langu,Malaika,Hii Leo,Nitakufaje,Miiko 10 ya Rap, Nitakupa Nini Mama.
Elimu Dunia
Akiwa kijana mdogo kabisa tena akiwa ametoka kwenye moja kati ya kundi bora zaidi kwenye Bongo Flava, Daz Mwalimu alikutana na P.Funk Majani na kutoka pale kila kitu kilibadilika kwenye maisha yake ya kimuziki. Pengine ni moja kati ya makosa yake makubwa aliyowahi kuyafanya lakini usingekuwa karibu kuwaza namna hiyo ikiwa nyimbo kama Namba 8, Wife, Elimu Dunia, Usihukumu zilikuwa na kiwango kikubwa mno na usingeweza kumlaumu kwa wakati ule.
Namba 8 akiwa na Fid Q ulikuwa ni wimbo wa taifa na hata ulipotoka Wife na mwana Ngwea nao ukafuata mkondo huo. Hatujui kwa uwazi nini kilitokea ila baada ya albaum ile kila kitu kilibadilika na Daz Baba hakuwa kwenye ubora wake tena mpaka leo hii amegeuka kuwa mwanamuziki wa kawaida pamoja ukubwa wa album hiyo. Mwaka 2004 ndio ilienda hewani album hii ya kukumbukwa.
Safari
Ferooz na sauti yake ya kulalamika alikuwa kwenye ubora mkubwa mno kipindi hiki. Ni mmoja kati ya watu walioibeba Daz Nundaz kwa mabega yao na usingebisha hili ukijua kuwa nyimbo kama Barua na Kamanda ni nyimbo zilizokuwa na sauti yake zaidi kuliko member wenzie wa kundi lile.
Alirudi tena akiwa na peke yake na ngoma yake ya kwanza ya Jirushe akiwa na Jay Moe kutoka pale Bongo Records kwa P.Funk. Haikuchukua muda akadondosha wimbo bora zaidi katika maisha yake, Starehe. Hatujakaa vizuri akatuletea Wema Wangu Umeniponza na ngoma nyingine nyingi kubwa kwenda kukamilisha album hii ilioacha historia kubwa kwenye Bongo Flava.
Raha Kamili
AY alikuja Dar es Salaam kama kutoka Morogoro kutafuta maisha akiwa na begi lake tu. Hakuwa na ndugu wala jamaa wa karibu zaidi ya washkaji zake Buff G na Snare aliosoma nao Ifunda Sekondari. Yeye, Buff G na Snare walianzisha kundi lao la SOG. Nyimbo za SOG zililigusa sikio la P-Funk aliyemwalika kwenye studio zake na kutengeneza ngoma yake iliyompa jina zaidi, Raha tu.
Mwaka 2001, aliachia album yake Raha Kamili iliyojumuisha nyimbo kama Safi Hiyo, Ni Alfajiri, Machoni kama watu (ft. Lady JD), Ni raha tu (feat. Complex), Msimamo wako, Nachotaka uelewe, Mchango wa macho, Raha kamili, Sio kila Siku na zingine.
Machozi, Jasho na Damu
Profesa Jay aka Heavy weight MC, Wa mitulinga, Mchawi wa Rhymes, Mti Mkavu, ni msanii wa Bongo Flava mwenye hit songs nyingi zaidi.
Baada ya kuvunjika kwa HBC,Profesa Jay aliamua kuendelea na game na hii ilikuwa album yake ya kwanza akiwa kama msanii huru mwaka 2001. Bongo Dar es Salaam ni wimbo fulani ambao Jay alizungumzia ujanja ujanja wa bongo na kila mtu akiwa tapeli hata muhuri wa ikulu unapata, bila matata na suala la kupewa pesa bandia baada ya kuuza cheni bandia ni kawaida mno ndani ya Bongo. Wimbo kama Niamini alioimba na washkaji zake Terry Fanani na Big Will ulikuwemo kwenye album hii pia.
Ndio Mzee, Jina langu, Piga Makofi na Salamu Babu na Bibi zilikuwa ni nyimbo nyingine zilizoshiba kwenye album hii ya kibabe.
Nyimbo zingine ni pamoja na Nawakilisha, Yataka Moyo, Piga Makofi na Tathmini.
Fid Q aliwahi kusema Machozi, Jasho na Damu ni album bora ya karne. “#MachoziJashoNaDamu is an indisputable/classic/dope/great&prolly the best album of the 1st century,” aliandika Fid kwenye Twitter.
P.Funk Majani ni producer aliyefanya ngoma nyingi zaidi kwenye album hii.

Ipi kati ya hizi ni album bora zaidi kwako?
Tazama video hapa chini..

No comments

+255716829257