Habari mpya

UJASIRIAMALI NI MTAJI JE UNASADIKI HILO??

Image result for UJASIRIAMALI NI MTAJI JE UNASADIKI HILO??
Elimu ya ujasiriamali ni mtaji mkubwa wa kujinasua na umaskini, ingawa upatikanaji wake umekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana wengi, na ndio maana wamekuwa na woga wa hata kuthubutu kujiingiza katika mikataba ya mikopo kutoka taasisi za fedha, wanachoogopa ni namna ya kuzizalisha kwa faida ili kujihakikishia uwezo wa kuzirejesha.

Serikali imekuwa ikiwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kuwapatia mikopo, kilichopunguza kasi ya kuanzisha vikundi hivyo ni kukosa elimu ya ujasiriamali, wananchi wanashindwa kujua mikakati ya uzalishaji wakiwa kama kikundi.

Miaka ya nyuma kabisa, serikali iliwahi kuwapelekea ng'ombe wananchi wa baadhi ya mikoa ya Kusini ili wafuge na kunufaika kwa maziwa, ngozi, mbolea nk. Kutokana na kukosa elimu, wananchi hao walikaa katika vikundi vyao na kufanya maamuzi ya kuwachinja kwa awamu na kufaidi nyama, wakidai kuwa yalikuwa maamuzi ya msingi.

Kulikuwepo na mzunguko wa fedha huko mikoani zilizotolewa na Rais Kikwete na zikajulikana kama 'Mabilioni ya JK', fedha hizo zilitolewa kwa nia njema ya kuwakopesha wananchi ili iwe mitaji yao kuanzisha miradi ya kujikimu kimaisha. 

Utaratibu wa kukopeshana haukuwa mzuri, kwani walionufaika ni wachache mno na baadhi yao walizitafuna kama walivyofanya kwa ng'ombe huko Kusini.

Serikali imeamua kuwekeza fedha zaidi katika Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi, ni katika mpango ule ule wa Mabilioni ya JK, ambapo safari hii serikali imedhamiria kuweka mpango mzuri wa utoaji wa fedha hizo. 

Tayoa inaamini kuwa umuhimu wa kuwawezesha vijana kuwa wajasiriamali wenye maarifa ya kutosha ni kuwawezesha kushindana na watu wengine duniani kwani wanaamini msingi mkubwa wa ujuzi na maarifa kwa vijana ni lazima utokane na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizindua mradi wa Tayoa mwanzoni mwa wiki hii alisema Tayoa iko katika nafasi nzuri ya kuleta mabadiliko yanayotarajiwa kwa jamii na vijana hasa katika utoaji wa maarifa muhimu.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Tayoa, Peter Masika, alisema kufuatia kuongezeka kwa tatizo la ajira kwa vijana, ambako alisema kumesababishwa na ukosefu wa ujuzi wa kuanzisha na kuisimamia biashara, Tayoa iliamua kuanzisha shule ya kuwaelimisha vijana namna ya kujiajiri.

Kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu aliipongeza NBC kwa kushirikiana na Tayoa kwa kuandaa na kufanikisha mafunzo ya ajira na ujasiriamali kwa vijana, ambapo alisema mchango wa NBC utasaidia kupunguza umaskini hasa kwa vijana na watoto.


Maisha ya vijana wengi sasa yanalenga katika mfumo wa kujiajiri zaidi kuliko kusubiri ajira, na ndio maana wakati mwingine ni busara kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuongeza somo la elimu ya ujasiriamali kwa wanaohitimu. Itawajengea hisia ya kujiandaa zaidi kisaikolojia kabla ya kuingia mitaani

No comments

+255716829257