EPUKA UGONJWA WA KISUKARI KWA KUFANYA HAYA…
Ugonjwa wa kisukari unaongezeka
haraka sana hivi kwamba umekuwa janga la ulimwenguni pote. Kuna aina mbili kuu
za kisukari. Aina ya kwanza huanza hasa utotoni ambayo kufikia sasa madaktari
hawajui jinsi ya kuizuia.
Ingawa zamani aina ya pili ya kisukari ilihusianishwa tu na
watu wazima, hivi karibuni imewaathiri pia watoto. Lakini wataalamu wanasema
kwamba mtu anaweza kujikinga ili asipatwe na kisukari. Huenda ukafaidika kujua
habari fulani kuhusu ugonjwa huu hatari. *
Kisukari Ni Nini?
Kisukari ni ugonjwa unaotokana na
mtu kuwa na sukari nyingi kupita kiasi kwenye damu. Ugonjwa huo huvuruga
utaratibu wa kuingiza sukari ndani ya chembe kutoka kwenye damu kwa kuwa chembe
huhitaji sukari ili kupata nishati. Matokeo ni kuharibiwa kwa viungo muhimu na
hitilafu ya mzunguko wa damu, na nyakati nyingine unaweza kufanya mtu akatwe
vidole vya miguu au mguu, pia husababisha upofu, na maradhi ya figo. Wagonjwa
wengi wa kisukari hufa kutokana na mshtuko wa moyo au kiharusi.
Mafuta mengi kupita kiasi mwilini
huchangia sana kisukari. Wataalamu wanaamini kwamba mafuta yaliyokusanyika
tumboni na kiunoni ni ishara ya uwezekano wa kupatwa na kisukari. Kihususa,
mafuta katika kongosho na ini huvuruga uwezo wa mwili wa kudhibiti kiasi cha
sukari kwenye damu. Unawezaje kuepuka kupatwa na kisukari?
Hatua Tatu Zinazoweza
Kukusaidia Usipatwe na Kisukari
1. Pimwa
kiwango cha sukari kwenye damu ikiwa una uwezekano mkubwa wa kupata
kisukari. Mara nyingi aina ya pili ya kisukari huanza baada ya hatua
inayoitwa prediabetes, yaani, ongezeko la kiwango cha sukari
kwenye damu. Hatua hiyo ni hatari kama tu kisukari, lakini kuna tofauti: Ingawa
ugonjwa wa kisukari unaweza kudhibitiwa, hauwezi kutibiwa. Kwa upande mwingine,
watu walio na kiwango cha juu cha sukari kwenye damu wamefaulu kukipunguza.
Huenda mtu asitambue dalili za ongezeko la sukari kwenye damu. Kulingana na
ripoti mbalimbali, karibu watu milioni 316 duniani pote wana kiwango kikubwa
cha sukari kwenye damu; ingawa wengi wao hawajui wana kiwango hicho. Kwa mfano,
nchini Marekani pekee asilimia 90 ya watu wenye sukari nyingi kwenye damu
hawatambui kama wana tatizo hilo.
Ingawa hivyo, ongezeko la sukari kwenye damu ni hatari.
Mbali na kuwa kisababishi cha kisukari, hali hiyo imehusianishwa na hatari ya
kupatwa na ugonjwa wa akili uitwao dementia. Kama wewe ni
mnene kupita kiasi, hufanyi mazoezi kwa ukawaida, au una watu wa ukoo walio na
kisukari, huenda tayari una kiwango cha juu cha sukari kwenye damu. Unaweza
kujua kiwango chako cha sukari ukipimwa damu.
2. Kula
vyakula vyenye lishe. Unaweza kufaidika ukifanya mambo yafuatayo:
Punguza kiasi cha chakula unachokula. Badala ya kunywa vinywaji vyenye sukari
nyingi au vinywaji vyenye kaboni kama vile soda, kunywa maji, chai, au kahawa.
Kula vyakula vya nafaka ambayo haijakobolewa badala ya vyakula vilivyochujwa
sana viwandani. Kula nyama isiyo na mafuta mengi, samaki, njugu, karanga, na
maharagwe.
3. Fanya
mazoezi. Kufanya mazoezi kunaweza kupunguza kiwango cha sukari kwenye
damu na kukusaidia uwe na uzito unaofaa. Mtaalamu fulani anapendekeza kupunguza
muda unaotumia kutazama televisheni ili uwe na muda wa kufanya mazoezi.
Huwezi kubadili chembe zako za
urithi, lakini unaweza kubadili maisha yako. Utafaidika sana ikiwa utajitahidi
kutunza afya yako.
picha na mzizi mkavu.
No comments
+255716829257