Habari mpya

MAREKANI KUONGEZA WANAJESHI SUDAN KUSINI..

Mapigano
Marekani imesema itawatuma wanajeshi 40 zaidi Sudan Kusini kusaidia kulinda Wamarekani na mali ya Marekani mjini Juba.
Msemaji wa jeshi la Marekani barani Afrika, Africom, Jennifer Dyrcz amesema wanajeshi hao wa Marekani wametumwa nchini humo baada ya mapigano yaliyoanza wiki iliyopita.
Kwa sasa hali imetulia baada ya Rais Salva Kiir na Makamu wa Rais Riek Machar kuagiza wanajeshi wao wasitishe vita Jumatatu.
Ubalozi wa Marekani mjini Juba, kwa mujibu wa shirika la habari la AP, umesema raia wa Marekani wanaotaka kuondoka Sudan Kusini watasaidiwa kuondoka kwa ndege.
Wafanyakazi wasio muhimu sana katika ubalozi huo pia wataondolewa.
Mashirika makubwa ya ndege yalisitisha safari za ndege kutua na kupaa kutoka Juba.
Safari za ndege za kibinafsi na za kukodisha hata hivyo zimerejelewa na ndege hizo zinatumiwa kuwaondoa wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada pamoja na raia wa kigeni kutoka Juba.
Umoja wa Mataifa umesema raia 36,000 wa Sudan Kusini wametoroka makwao kutokana na mapigano na kutafuta hifadhi makanisani, katika kambi za UN na kambi za mashirika ya kutoa misaada.

Image copyrightAFP

Taarifa zinasema serikali ya India pia imefanya mipango ya kuwaondoa raia wake kutoka nchini humo kwa kutumia ndege Julai 14.
"Safari zaidi zitapangwa baadaye kukiwepo na hitaji,” tovuti ya habari ya Tamazuj imesema, ikunukuu taarifa kutoka ubalozi wa India nchini Sudan Kusini.

No comments

+255716829257