ZIJUE FAIDA ZA KIPORO..
Je wewe unapenda kiporo? Basi leo nna habari njema juu ya kiporo
unachokula.Tamaa kubwa ya watu wengi iko kwenye chakula. Wengi tunapenda kula
vizuri kuliko kitu kingine chochote kile maishani. Ukiangalia uswahilini kwetu
ugomvi mkubwa huanzia kwenye chakula, ndoa huanza kupata nyufa kutokana na
chakula na mengine mengi tu yanaanzia kwenye chakula.
Mie nadhani hii inatokana na ukweli
kuwa chakula ndio kitu pekee kinachoweza kumfanya mtu ajisikie vizuri katika
ngazi yeyote ile ya maisha. Ukila vizuri unajisikia vizuri na afya tele, hata
kama ni mara moja kwa mwaka. Lakini kuna tatizo kwenye kupenda sana kula, hasa
vile vyakula visivyofaa kwa matumizi ya binadamu, utaishia kuongeza uzito ambao
una madhara makubwa kwenye afya yako.
Lakini leo hatuzungumzii kula
vizuri, wala kunenepa, bali tunaangalia njia ya kula chakula vizuri na kuwa na
uhakika wa kutoongeza kalori (carolies) nyingi mwilini, hivyo kukufanya uwe na
afya zaidi. Na mada yetu inahusu zaidi kwenye kula viporo - iwe
wali maharage, tambi au vyakula vingine vingi.
Kula vyakula vilivyotoka kuandaliwa
ni salama na afya zaidi, hii haina ulazima wa ufafanuzi. Lakini kuna jamii ya
vyakula ambavyo ni vizuri zaidi kula vikiwa kama viporo. Aina mojawapo muhimu
sana la hivi vyakula ni kundi la vyakula vya wanga (carbohydrates).
Tunakula vyakula vya wanga mara
nyingi sana kwenye milo yetu ya kila siku. Ukila vyakula vya jamii ya wanga
unaongeza kiwango cha sukari kwa kasi sana kwenye damu, wakati wa mmeng'enyo,
hivyo hulazimu mwili kufanya kazi ya ziada ya kutoa kimeng'enyo cha insulin kinachofanya
kazi ya kupunguza sukari kwenye damu. Hii kupanda na kushuka kwa damu kwa kasi
husababisha chakula kusagwa haraka sana na unaweza kusikia njaa muda mfupi
baada ya kula. Hii pia ni jibu mojawapo kwanini unasikia usingizi ukiwa umetoka
kula chakula cha wanga - sukari na mwili kufanya kazi kwa nguvu - hukufanya
kuwa na uchovu na uvivu.
Lakini, leo nna habari tofauti.
Imefanyika utafiti na inaonyesha kuwa kuna utofauti wa umeng'enyaji kati ya wanga
uliopikwa (wa mtoto), uliopoa na ule uliopoa na kupashwa moto. Hii ni kutokana
na utafiti uliofanywa na kuripotiwa na BBC . Utafiti unaonyesha kuwa
kiwango cha mmeng'enyo na sukari kwenye damu kinapungua kama wanga ikipikwa na
kuliwa kama kiporo (baridi), lakini hupunguza zaidi kiwango cha sukari kwa
asililia 50% kama ikiwa kiporo na kupashwa moto. Hii ni kutokana na virutubisho
vingi kutomeng'enyeka kirahisi baada ya wanga kupoa na kupashwa moto. Utafiti
huu ulifanywa kwa kutumia tambi, lakini hii ni tabi aya vyakula vingi aina ya
wanga.
Hii inamaanisha nini kwako wewe
mlaji?
Utafiti huu unatoa ufafanuzi mzuri
juu ya vyakula tunavyokula. Kutokana na matokeo haya, ni vizuri zaidi kula na
kushiba kiporo cha jamii ya wanga sababu hakitokufanya uongezeke uzito kama
utakapokula chakula cha kawaida. Hii ni kwa sababu nusu ya chakula unachokula
ndio kinachotumika kukupa karoli mwilini na kilichobaki huishia kutoka kama
makapi.
Watu wengi sana wanapenda kupunguza
uzito bila kuvuruga kula, hii inawezekana kama utafanya mazoezi magumu na ya
muda mrefu. Lakini kwa kupata matokeo mazuri zaidi, kupunguza kula vyakula
visivyo na afya ni kitu muhimu zaidi kuliko hata mazoezi. Nasema hivi sababu
chakula ndio kinachokufanya uongezeke uzito, lakini si swala la kujinyima kula,
ni swala la kujua jinsi ya kula vyakula visivyokufanya unenepe. Vyakula vya
kuzuia ni chumvi, sukari, na mafuta yasiyo na afya kama yalivyoelezewa hapa. Lakini leo
unaongeza kiporo kwenye orodha ya vyakula vya kula bila kuwa na wasiwasi wa
kunenepa.
Unaweza kuwa na swali, je
kwanini ukila kiporo huwa nahisi kuvimbiwa na tumbo kujaa? Jibu ni rahisi,
na sababu pekee ni kuwa unakosea kupasha moto kiporo chako, na jibu liko hapa
chini. Lakini kwanza tuangalie jinsi ya kuhifadhi kiporo.
Je
unahifadhi vipi kiporo ?
Ili kuzuia madhara ya kula chakula
kisicho bora, kuwa makini kwenye kuhifadhi chakula vizuri. Ili kuhifadhi
chakula chochote ni lazima kukiweka kwenye mazingira yanayozuia wadudu
kuzaliana. Hivyo basi, ili kulinda chakula muda mrefu na kuepukana na madhara
ya kuingiwa na vijidudu vinavyoweza kuleta sumu, weka chakula kwenye jokofu
mara tu baada ya kumaliza kula. Vyakula vingi huharibika haraka na kuingiwa na
wadudu mara tu vikishapoa, hasa vyakula vyenye protini ambavyo huharibika
haraka sana vikihifadhiwa vibaya. Ni vizuri kulinda afya yako kwa kuhakikisha
chakula kimehifadhiwa vizuri ili kuweza kuliwa wakati kinapohitajika.
Jinsi
ya kupasha moto kiporo
Inawezekana ukaona ni swali lisilo
na msingi, lakini mara nyingi wengi wetu hatufahamu jinsi ya kupasha moto
kiporo. Wengi huweka jikoni na kuwa na papara ya kula kabla hakijapata moto
vizuri. Hii si sawa, sababu kila chakula huwa na masharti yake kwenye kupasha
moto. Moto husaidia kuamsha virutubisho na vilevile kuua vijidudu
vilivyozaliana kwenye chakula.
Ukiwa unapasha moto kiporo cha wali,
ni vizuri ukakiweka jikoni muda mrfu ili kipate moto vizuri. Hii ni muhimu
sana, siyo tu kuua vijidudu, bali hukuwezesha kupata urahisi kwenye kukisaga
chakula tumboni.
Chakula kikiwa hakijapata vizuri
moto hukufanya kujisikia uvivu na hamu ya kulala. Ndio maana mara nyingi
watu wengi huingiwa na uvivu na kupenda kulala baada ya kula kiporo kizito cha
wali maharage asubuhi. Mie pia imeshanitokea mara nyingi na huwa napenda sana
kiporo cha ubwabwa maharage, hasa yakiwa ya nazi.
Njia nzuri ya kuhakikisha unapasha
moto chakula vizuri ni kuwa na microwave.
Pasha moto kwa muda usiopungua dakika 4 ili kupata matokeo mazuri. Kama
unatumia jiko la kawaida, ni vizuri ukaweka jikoni kwa muda na kuhakikisha
chakula kinapata moto vizuri kabla ya kukitenga na kula.
No comments
+255716829257