Habari mpya

BUNGE: KIDOLE CHA KATI CHAMPONZA SUGU..

 
Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu amehukumiwa adhabu ya kukosa vikao kumi vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Alhamis hii, June 30 kutokana na kosa la kunyoosha kidole cha kati wakati akitoka bungeni.
Akiwasilisha hukumu hiyo bungeni, mwenyekiti wa kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika alisema, “Mnamo tarehe 13 mwezi wa sita ulifikisha mbele ya kamati yangu shauri la Mheshimiwa Joseph Mbilinyi ambaye alilalamikiwa kutoa ishara ya matusi bungeni ili kamati iweze kuchunguza na kutoa mapendekezo kwa mujibu wa kanuni.”
Akitaja chimbuko la malalamiko hayo, Mhe Mkuchika alisema kuwa Juni, 6 mwaka huu kwenye kikao cha 37, mkutano wa tatu, kwenye Bunge la 11, Mbunge Jacquline Msongozi aliomba muongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya 68,7 ya kanuni za kudumu za Bunge, Mhe. Msongozi alieleza kuwa Mhe. Joseph Mbilinyi ambaye ni msemaji mkuu wa kambi ya upinzani baada ya kuwasilisha taarifa ya kamati sanaa, ubunifu, utamaduni na michezo iliyohusu azimio la Bunge la kuridhia mkataba wa kimataifa wa kudhibiti madawa na mbinu ya kuongeza nguvu michezoni, wakati anatoka alionyesha kidole chake cha kati juu cha mkono wa kulia huku vidole vingine akiwa amevikunja ikiwa ni ishara ya matusi.
Aidha muongozo huo wa Mhe. Msongozi uliungwa mkono na Mhe. Sixtus Mapunda, baada ya kupewa nafasi ya kusema muongozo wake alilieleza Bunge kuwa muongozo wake ulikuwa unahusu jambo hilo hilo lililoombewa muongozo na Mhe. Msongozi. Baada ya maombi ya miongozo hiyo Mhe. Spika alieleza Bunge kuwa hajakiona kitendo hicho alichokifanya Mhe. Mbilinyi lakini atalifuatilia suala hilo na kisha atalichukulia hatua.
Kamati ilikusanya ushahidi kwa kuwaita kwa kutumia hati za wito. Kamati ilifanya rejea katika nyaraka na ushahidi uliotolewa na mashahidi mbele ya kamati. Nyaraka zilizotolewa ni pamoja na Sheria ya kinga na madaraka ya Bunge sura ya 296, Kanuni za kudumu za Bunge, toleo la Januari 2006, picha ya video ya tarehe 26 Juni 2006, ushahidi wa Mhe. Mbilinyi, Msongozi na Mapunda.
“Katika maelezo ya Mhe. Jacquline Msongozi alieleza kuwa alimuona kwa macho yake Mhe. Mbilinyi akionyesha kidole chake cha kati kwa mkono wa kulia kwa uelekeo wa kwenda juu, ishara kwa utamaduni wa kimataifa na jamii ya kitanzania ni tusi. Aliendelea kueleza kuwa maana yake kuingiliwa kinyume na maumbile kwa mwanamke au mwanaume, hivyo ishara hiyo imemfedhehesha akiwa kama mwanamke na Mbunge wa Bunge la muungano,” alisema Mkuchika.
Aliongeza kwa kusema, “Shahidi mwingine alikuwa Mhe. Sixtus Mapunda ambaye alieleza kuwa alimuona Mhe. Mbilinyi akinyoosha kidole chake cha kati ishara ambayo ni tusi. Alipohojiwa maana ya ishara hiyo naye alieleza kuwa ni tusi lenye maana ya kuingiliwa kinyume na maumbile.”
Mheshimiwa Mkuchika aliendelea kwa kusema kuwa Mhe. Mbilinyi aliitwa na kamati hiyo Juni 16, 2016 ili kutoa ushahidi wake kuhusu tuhuma zilizomkabili na kudai kuwa wakati anakaribia mlango wa kutoka bungeni alisikia sauti ya Mbunge wa CCM akimtukana matusi ya nguoni kwa kumtukana mama yake, hivyo inawezekana alinyoosha kidole hicho cha kati kutokana na hasira aliyokuwa nayo baada ya kusikia akitukanwa.
Kwenye ushahidi wake Mhe. Mbilinyi aliongeza maana ya ishara hiyo, alidai kuwa lugha ya ishara huwa haina maana ya moja kwa moja na kwa uelewa wake hiyo ni alama ya kupinga jambo lililotokea.
Mhe. Mkuchika alinukuu ushahidi wa Mhe. Sugu kwa kusema, “Nakumbuka nilionyesha mkono wa vidole viwili ambayo ni body direction, kidole cha kati ni resistance sign inawezekana nilinyoosha kidole cha kati kwa sababu ya temper.”
Aidha kamati hiyo katika kutafuta ushahidi wa kujiridhisha zaidi juu ya ishara hiyo kama ni tusi au siyo kwa kupitia baadhi ya vitabu hukumu zilizowahi kutolewa juu ya watu waliowahi kuonyesha ishara hiyo ikiwemo aliyekuwa mchezaji wa Liveerpool, Luis Suarez tarehe 28,12 2011 alipewa adhabu ya kufungiwa mechi moja na kutakiwa kulipa faini ya paundi elfu ishirini kutokana na kosa la kuwanyooshea mashabiki wa timu ya Fulham kidole hicho cha kati. Nacho kitabu cha ‘The Divinitive Book Body Of Language’ kilichoandikwa na Allan na Barbara, kilichochapishwa na kampuni ya Clave ya Uingereza mwaka 2004, kwa utamaduni wa kimarekani ishara hiyo inamaanisha kuwa “Sit on this, screw you.”
Kutokana na ushahidi huo, Sugu alipewa adhabu hiyo ya kutohudhuria vikao 10 vya bunge.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Said Kubenea amehukumiwa adhabu ya kutoshiriki kwenye vikao vitano vya Bunge kuanzia leo tarehe 30 mwezi 6 mpaka vitakapotimia vikao hivyo vitano kwa kosa la kutoa maneno yasiyo na ukweli na kushindwa kumuomba radhi Waziri Hussein Mwinyi.
chanzo: Bongo5

No comments

+255716829257