Watu kufanya kazi siku mbili kwa wiki Venezuela
Serikali ya Venezuela imeagiza wafanyakazi wake wawe wakifanya kazi siku mbili kwa wiki.
Hii ni hatua ya muda iliyochukuliwa kutokana na uhaba wa umeme.
Makamu wa Rais Aristobulo Isturiz ametangaza kwamba watumishi wa umma wanafaa kufika kazini Jumatatu na Jumanne pekee hadi mzozo wa sasa wa nishati umalizike.
Venezuela imekabiliwa na ukame mkubwa ambao umepunguza maji kwenye bwawa lake kuu la kufulia umeme.
Lakini upinzani umeituhumu serikali kwa kutodhibiti vyema mzozo wa sasa.
Agizo la kupunguzwa kwa siku za kufanya kazi, lililotolewa kupitia runinga ya taifa na Bw Isturiz, litaathiri watu milioni mbili wanaofanya kazi serikali.
"Hakutafanywa kazi katika sekta ya umma Jumatano, Alhamisi na Ijumaa, ila tu majukumu muhimu sana,” alisema.
Rais Nicolas Maduro alikuwa tayari amewaruhusu wafanyakazi 2.8 milioni wa serikali nchini humo kutofanya kazi Ijumaa mwezi Aprili an Mei, ili kupunguza matumizi ya umeme.
Amesema Venezuela imeathiriwa sana na hali ya hewa ya El Nino na kwamba hali ya kawaida itarejea baada ya mvua kuanza kunyesha.
Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kupunguza matumizi ya umeme.
Februari, maduka yaliagizwa kupunguza muda ambao yanafunguliwa kila siku na pia kujaribu kujizalishia umeme.
Mapema wiki hii, serikali pia ilisongeza mbele saa kwa nusu saa ili kupunguza mahitaji ya umeme kwa ajili ya mwanga mapema jioni.
Chanzo: BBC
No comments
+255716829257