Habari mpya

Muhtasari: Habari kuu leo Alhamisi

1. UN yaanza kusaidia waathiriwa Syria

SyriaImage copyrightAFP
Image captionMapigano bado yanaendelea katika baadhi ya maeneo
Umoja wa Mataifa umeanza kutoa huduma za kibinadamu na kuwahamisha mamia ya watu wagonjwa na waliojeruhiwa, kuwaondosha kutoka miji iliyozingirwa na vikosi vya serikali ya Syria vinavyopambana na waasi.
Ni maeneo ambako kulikuwa na mkataba wa kusitisha mapigano lakini huwa inakiukwa mara kwa mara.

2. Mlipuko wa kemikali waua watu Mexico

Watatu
Image captionWatu watatu wamefariki
Kumetokea mlipuko katika kiwanda cha kemikali huko kusini mashariki mwa Mexico uliowauwa watu watatu na wengine 100 kukimbizwa hospitalini.
Moshi mkubwa mwenye kemikali zinazodhuru afya ulitanda katika mji wa bandari wa Coatza-coalcos na ikabidi shule na majengo ya biashara kufungwa. Sasa mkasa huo unachunguzwa.
Shirika la Serikali la mafuta Pemex linamiliki nusu ya kiwanda hicho

3. Majeshi ya El Salvador kukabili magenge

SanchezImage copyrightGetty
Image captionRais wa El Salvador Sanchez Ceren
Serikali ya El Salvador imesema inapeleka kikosi kipya kikubwa cha wanajeshi na polisi kupambana na magenge ambayo sasa yanafanya uhalifu vijijini baada ya kutoroka operesheni kali dhidi yao katika maeneo ya mijini.
El Salvador ni mojawapo ya nchi zilizo na viwango vikubwa vya uhalifu hasa mauaji yanayoendelezwa na vita baina ya magenge yapatayo elfu 70 nchini humo.
Waziri wa ulinzi nchini humo amesema watatumia helkopta, magari ya kivita na silaha kali kuwasaka viongozi zaidi ya mia moja wa magenge hayo.

4. Mazungumzo ya amani kuanza Yemen

waasiImage copyrightReuters
Image captionMakundi ya waasi yalisusia mazungumzo Jumatatu
Mazungumzo ya kutafuta amani na kumaliza vita nchini Yemen yanatarajiwa kuanza tena leo huko Kuwait.
Yalikuwa yafanyike Jumatatu iliyopita lakini yakakwamishwa kwa sababu ya kususiwa na wawakilishi wa waasi wa Houthi wanaolalamikia kuvunjwa kwa makubaliano ya kusitisha uhasama.

5. Polisi wakiri kuua raia New Orleans

MafurikoImage copyrightAP
Image captionMafuriko yaliyosababishwa na kimbunga cha Katrina
Maafisa watano wa polisi huko New Orleans Marekani wamekiri mashtaka kuhusiana na tukio la kuawa kwa raia wawili kwa kufyatuliwa risasi siku chache baada ya mkasa wa mafuriko yaliyosababishwa na gharika ya Katrina hapo 2005.
Watu hao wawili walikuwa wakitembea wakivuka daraja wakati walipopigwa risasi pasi na kufanya kosa lolote.

6. Australia yaweka mkakati wa kukabili wadukuzi

MtandaoImage copyrightAFP
Image captionAustralia inataka pia kuwa ikijibu wanaoishambulia mtandaoni
Australia inatarajia kuwa na mfumo wa kukabiliana na mashambulio ya wadukuzi katika mitandao baada ya kuanzisha mkakati mpya utakaoigharimu zaidi ya dola millioni 220. Zaidi ya hayo wataalamu hao wa Australia wanasema mfumo pia utawawezesha sio tu kuzuia bali pia kuwashambulia wafanya hujuma za mitandaoni.

7. Picha ya mtumwa kuwekwa kwenye dola

TubmanImage copyrightAFP Women On 20s
Image captionTubman alisaidia watumwa wengi kujipatia uhuru
Picha ya mtumwa mmoja aliyekata nyororo na kisha kusaidia mamia ya wenzake kutoroka utumwa sasa itatumika katika noti mpya ya dola 20 nchini Marekani. Mwanamke huyo Harriet Tubman atakuwa Mwafrika Mmarekani wa kwanza ambae picha yake imewekwa kwenye sarafu ya Marekani.

8. Malkia Elizabeth atimiza miaka 90

ElizabethImage copyrightAFP
Image captionMalkia Elizabeth alizaliwa 21 Aprili, 1926
Malkia wa Uingereza Bi Elizabeth anasherehekea siku yake ya kuzaliwa - akiwa na umri wa miaka 90. Anaingia katika kumbukumbu za kihistoria kwa kuweka rekodi ya utawala wa zaidi ya miaka 64.

9. Urusi yataka kukubaliwa kushiriki Olimpiki Rio

UrusiImage copyrightepa
Image captionBw Mutko. Urusi ilizuiwa kushiriki mashindano ya kimataifa ya riadha kwa sababu ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli
Na Urusi imetangaza hatua yake ya kuushawishi uongozi chama cha riadha Duniani ili wachezaji wake waruhusiwe kushiriki katika mashindano ya Olympiki ya Rio mwaka ujao.
Waziri wa michezo, Vitaly Mutko amesema kuwa kwa wale wote wenye nia ya kushiriki michuano hiyo watatakiwa kufanyiwa uchunguzi huru mara tatu kabla.

10. Canada yataka kuhalalisha bangi

BangiImage copyrightAFP
Image captionTrudeau aliahidi kuhalalisha matumizi ya bangi
Serikali ya Canada imesema itatimiza moja ya ahadi za Waziri Mkuu Justin Trudeau wakati wa kampeni na kupeleka bungeni mswada ambao huenda ukapelekea kuhalalishwa kwa bangi. Mswada huo utajadiliwa majira ya kuchipua mwaka ujao.
Serikali inasema itashirikiana na polisi kudhibiti uuzaji wake katika kufuatilia ni nani anauziwa, inauzwa wakati gani na inatumiwa vipi. Upinzani wenye wahafidhina wengi unasema kuhalalishwa kwa bangi kutawadhuru vijana.

No comments

+255716829257