Obama: Trump hatakuwa rais Marekani
Rais Barack Obama amesema anaamini mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump hatakuwa rais wa Marekani.
Amesema kazi hiyo ni “kazi kubwa”.
"Ninaendelea kuamini kwamba Bw Trump hatakuwa rais. Na sababu ni kwamba nina imani sana na Wamarekani,” amesema Bw Obama.
Bw Trump, mfanyabiashara tajiri sana kutoka New York, anaongoza kwenye kura za maoni katika kinyang’anyiro cha kuteua mgombea wa chama cha Republican.
- Trump alidhani mji wa Paris uko Ujerumani?
- Wabunge Uingereza wamjadili Trump
- Wagombea wamkejeli Trump kwenye mdahalo
Tayari ameshinda uchaguzi wa mchujo jimbo moja, na anaongoza kwenye kura za maoni jimbo la South Carolina, ambako wafuasi wa Republicans watashiriki uchaguzi wa mchujo Jumamosi.
Akiongea wakati wa mkutano mkuu wa kiuchumi wa nchi za kusini mashariki mwa Asia unaofanyika katika jimbo la California, rais aliulizwa na mwanahabari kumhusu Trump.
Watu hawatampigia kura, alisema Bw Obama, kwa sababu “wanajua kuwa rais ni kazi kubwa”.
"(Kazi hii ) Si kama kuzungumza katika kipindi cha runinga, si matangazo au mauzo ya bidhaa, ni kazi ngumu. Si kazi ya kushawishi watu na kufanya utakalo ndipo utokee kwenye vichwa vya habari siku fulani.”
Bw Trump amemjibu na kusema ni kama kusifiwa iwapo utakosolewa na rais ambaye ameharibu sana nchi.
Mwanasiasa huyo anamchukia sana Obama na miaka ya nyuma alizoea kumtaka atoe stakabadhi za kuthibitisha kwamba alizaliwa Marekani.
No comments
+255716829257