Habari mpya

Majengo ya shirika la utangazaji Kenya yatwaliwa

KBC
Image captionKBC imekabiliwa na matatizo ya kifedha miaka ya karibuni
Serikali ya Baraza la Jiji la Nairobi ilitwaa kwa muda majengo ya shirika la utangazaji la Kenya (KBC) Jumanne kutokana na kutolipiwa kodi.
Baraza hilo liliweka bango kubwa katika lango la majengo hayo kutangaza kwamba majengo hayo yalikuwa chini ya usimamizi wa baraza hilo.
"Wapangaji wote wanafaa kulipa kodi kwa Baraza la Jiji hadi malimbikizi ya kodi yalipwe,” tangazo la baraza hilo linasema.
Afisa wa masuala ya kifedha katika baraza hilo Maurice Okeri alisema baraza hilo linadai kodi ya jumla ya $20 milioni (Shilingi bilioni mbili za Kenya).
Pesa hizo ni malimbikizi ya kodi ya kuanzia mwaka 2008.
Bw Okeri alisema shirika hilo lilikuwa limeahidi kuwa lingekuwa likilipa Sh5 milioni kila mwezi mwaka 2014 lakini ahadi hiyo ilivunjwa baada ya kulipa Sh20 milioni pekee.
Baadaye Jumanne, maafisa wa baraza hilo walishauriana na wasimamizi wa KBC kwa muda kabla ya kuafikiana kuhusu kulipwa wa malimbikizi hayo.
Bw Okeri alisema shirika hilo lililipa Sh5 milioni kupitia hundi papo hapo na wahusika wakaahidi kukutana Jumanne wiki ijayo kwa mashauriano zaidi.
Alisema maafisa wa baraza wataandama mashirika mengine ambayo yamekosa kulipa kodi kwa baraza hilo yakiwemo Taasisi ya Utafiti wa Matibabu Kenya (Kemri), Shirika la Mawasiliano (Telkom) na Kampuni ya Umeme (Kenya Power).
Hii si mara ya kwanza kwa baraza hilo kutwaa usimamizi wa majengo jijini Nairobi kutokana na kutolipiwa kodi lakini huwa nadra sana kwa mashirika ya serikali kuandamwa.
Shirika hilo la utangazaji limekuwa likikabiliwa na matatizo ya kifedha miaka ya karibuni.

No comments

+255716829257