NCHI ZA AFRIKA ZASHINDANIWA NA SAUDI ARABIA NA IRANI.
Sudan imegonga vichwa vya habari wiki hii baada ya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na Iran.
Hii ni baada ya Saudi Arabia kuvunja uhusiano na Iran ikilalamikia kuvamiwa na kuchomwa moto kwa ubalozi wake mjini Tehran na waandamanaji wa Kishia.
Shambulio hilo kwenye ubalozi lilifanyika huku hali ya taharuki ikizidi kutokana na mauaji ya mhubiri wa Kishia Sheikh Nimr al-Nimr aliyekabiliwa na tuhuma za ugaidi.
Djibouti na Somalia pia zimechukua hatua kama hiyo huku Misri ikilaani vikali shambulio hilo. Sudan imemulikwa zaidi na vyombo vya habari kutokana na jinsi uhusiano kati yake na Iran umedorora kwa kasi.
Nchi hizo zilikuwa washirika wa karibu sana katika masuala ya kijeshi kati ya miaka ya 1990 na 2000 huku Iran ikiipa Sudan silaha na mafunzo ya kijeshi.
Hata hivyo uhusiano ulianza kudorora mwaka 2014 baada ya Sudan nchi pekee ya Kiafrika inayoongozwa na Sheria za Kiislamu za Kisuni kumtimua mwanadiplomasia wa Iran kwa kueneza Uislamu wa Kishia nchini humo.
Katika uhasama kati ya Saudi Arabia na Iran sasa ni bayana kwamba Sudan imo katika kambi ya Saudia. Majeshi yake yamo katika kikosi kinachoongozwa na Saudia kupigana na makundi ya Kishia nchini Yemen.
Inaelekea kwamba Sudana ambayo haina ushawishi mkubwa katika siasa za kimataifa inataka kuonyesha hatua ambazo iko radhi kuchukua ili kuonyesha ushirikiano wake na nchi hiyo.
Uchumi wa Sudan umeathirika pakubwa tangu kutengana na Sudan Kusini yenye utajiri wa mafuta mwaka 2011 na ina matumaini kuwa uhusiano wake na Saudia utaisaidia kujikwamua kiuchumi.
Somalia nayo inalenga uwekezaji baada ya zaidi ya miongo miwili ya mapigano yakiwemo mapambano yanayoendelea dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab wanaohusishwa na kundi la kigaidi la al-Qaeda
Maafisa nchini Somalia hivi karibuni wanaume wawili raia wa Iran katika kile kinachoonekana kuwa onyo kwa Iran kuacha kueneza Uislamu wa Kishia katika nchi hiyo yenye Wasuni wengi.
Saudia imeonyesha ukarimu mkubwa katika uwekezaji na kufadhili miradi ya Kiislamu katika nchi kadhaa za Afrika. Kwa hivyo sio jambo la kushangaza kwamba Saidi Arabia imetangaza kuwa zaidi ya nusu ya wanachama 34 wa muungano wa kijeshi wa Kiislamu iliyouunda ni kutoka nchi za Afrika. Nigeria ambayo ni mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta barani Afrika na ambayo imekuwa ikipambana na wanamgambo wa Boko Haram ni mmoja wa wanachama hao. Hata hivyo kwa mujibu wa ripoti ya shirika ka habari la Reuters Nigeria imekanusha kujiunga na muungano huo.
Huenda nchi hiyo ya Afrika Magharibi isiegemee upande wowote kwani kuna wafuasi wa madhehebu ya Shia na vuguvugu la Kiislamu la Kishia nchini humo(IMN) linaungwa mkono na Iran. Vuguvugu la IMN linafanya kampeni ya kuundwa kwa Jamuhuri ya Kiislamu inayofuata mienendo ya Iran nchini Nigeria na limehusika katika makabiliano na jeshi katika siku za hivi karibuni.
Kwa mujibu wa makundi ya kutetea haki za binadam wafuasi 300 wa vuguvugu hilo waliuawa na wanajeshi mwezi uliopita baada ya jeshi kulishtumu kwa jaribio la kumuua mkuu wa jeshi Luteni Generali Tukur Buratai. Jeshi la Nigeria lilikanusha kutekeleza mauaji hayo. Madai hayo na pia kuzuiliwa kwa kiongozi wa IMN Ibraheem Zakzaky, vilisababisha ghadhabu miongoni mwa jamii ya Washia na kuathiri uhusiano wa kidplomasia kati ya Iran na serikali ya Nigeria.
Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari - ambaye ni Mwislamu wa Kisuni - hatapendelea kuwepo taharuki za kidini hasa wakati huu majeshi yake yanapokabiliana na wanamgambo wa Boko Haram, ambao ni Wasuni wanaohusishwa na kundi la Islamic State.
Huenda Nigeria itatoa wito suluhu ipatikane kwa njia ya amani katika mzozo kati ya Saudi Arabia na Iran bila kuegemea upande wowote. Huenda nchi nyingine za Afrika hasa zenye idadi kubwa ya Wasuni zikafuata mkondo huo.
Source BBC....http://www.bbc.com/swahili/habari/2016/01/160108_saudi_iran_africa_scramble?ocid=socialflow_facebook
No comments
+255716829257