Habari mpya

PERUZI HABARI KUU ZA ULIMWENGU LEO JULY 25, 2016..

 1. Mhamiaji kutoka Syria ajilipua Ujerumani
 Ansbach
Wakuu katika maeneo ya Kusini mwa Ujerumani, wamesema kuwa mtu mmoja, anayedhaniwa kuwa mhamiaji kutoka Syria, amejilipua ndani ya baa, akajiua na kuwajeruhi watu wengine 12.
Mlipuko huo ulitokea katika mji wa Ansbach karibu na tamasha moja la muziki wa nje, maarufu katika eneo hilo.
Zaidi ya watu elfu mbili wameondolewa kutoka katika tamasha hilo, ambalo baadaye lilisitishwa. Baadhi ya maeneo ya mji huo wa Ansbach, yamezingirwa na walinda usalama.
Ni shambulio la tatu huko Bavaria, katika kipindi cha wiki moja.
 2. Wada yasikitishiwa na uamuzi wa kuhusu Urusi
 
Mamlaka kuu inayochunguza utumiaji wa dawa za kututumua misuli miongoni mwa wanariadha duniani (Wada), imesema kuwa imetamaushwa mno na viongozi wa kuu Olimpiki, ambao wamekataa kuidhinisha marufuku iliyotolewa ya kuwazuia wanariadha wote wa Urusi, kushiriki mashindano ya Olimpiki ya mwezi ujao huko Rio, nchini Brazil.
Rais wa Wada, anasema kuwa shirika hilo limeweka wazi mpango wa serikali wa kutumia dawa hizo zilizopigwa marufuku.
Amesema uamuzi wa kamati kuu ya Olimpiki, utayumbisha upatikanaji wa wanariadhaa walio wasafi, bila ya kutumia dawa hizo.

3. Mkutano wa kisiasa wafanyika kupinga mapinduzi Uturuki

 
Maelfu ya watu nchini Uturuki, wameshiriki katika mkutano wa kwanza wa vyama vyote vya kisiasa, kulaani waliopanga jaribio la mapinduzi nchini humo.
Mkutano huo uliopangwa na vyama vikuu vya upinzani, ulivijumuisha vyama vya The CHP, pamoja na wafuasi wa chama cha AK, chake Rais Erdogan.

4. Kiongozi wa Democratic Marekani kujiuzulu

 
Kiongozi wa kitaifa wa kamati kuu ya chama cha Democratic nchini Marekani, anajiandaa kujiuzulu, muda mfupi kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa wajumbe, wa kumteua rasmi mgombeaji wa kiti cha Urais wa chama hicho.
Uamuzi wa Debbie Wasserman Schultz, unafuatia kuvuja kwa barua pepe, zinazoashiria kuwa viongozi wa ndani wa chama hicho, walijaribu kuhujumu kampeni ya mpinzani wa Bi Hillary Clinton, Bernie Sanders.

5. Bloomberg kumuunga mkono Clinton

 
Meya wa zamani wa New York, Michael Bloomberg, anasemekana kujiandaa kutangaza hadharani kumuunga mkono Hillary Clinton, kuwania urais Marekani.
Gazeti la The New York Times, linasema kuwa, Bw Bloomberg, mwanasiasa wa zamani wa Republican, ambaye amekuwa akimkosoa pakubwa Donald Trump, atamuidhinisha Bi Clinton, katika mkutano wa wajumbe wa chama cha Democratic.

6. UN yafurahishwa na makubaliano Colombia

 
Na hatimaye Umoja wa mataifa umepokea vyema makubaliano kati ya serikali ya Colombia na waasi wa kundi la FARC, ya kuwapa hakikisho ya moja kwa moja wanawake, kama sehemu ya muafaka wa amani ulioafikiwa nchini Cuba.
Maafisa wa Umoja wa mataifa, wanasema kuwa pande zote mbili, zimekubaliana kuwa wanawake wapatiwe nafasi sawa ya kumiliki ardhi, baada ya muafaka wa mwisho wa makubaliano hayo kutiwa saini.

No comments

+255716829257