Habari mpya

HUU HAPA MSIMAMO WA SERIKALI JUU YA WANACHUO ZAIDI YA 7000 WALIOSIMAMISHWA MASOMO UDOM..

 [​IMG]
Serikali imetangaza orodha ya wanafunzi ambao watarejea kuendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) baada ya uchambuzi kumalizika na kupatikana idadi ya wanafunzi ambao wana sifa za kuendelea na masomo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alisema kuwa kwa kipindi chote walikuwa wakifanya uchambuzi ili kuona ni wanafunzi gani walikuwa na sifa za kusoma kozi hiyo maalum ambayo ilianzishwa kutokana na tatizo la walimu wa Sayansi.

Alisema kuwa programu hiyo ilikuwa inahitaji walimu ambao watakwenda kufundisha shule za sekondari lakini kulikuwa na wanafunzi 1,210 ambao walikuwa wanachukua stashahada ya ualimu wa shule za msingi ambao ni kinyume na malengo na 6,595 wakichukua stashahada ya kufundisha shule za sekondari.

“Baada ya hatua ya kuwaondoa wanafunzi chuoni kuchukuliwa, serikali ilifanya uchambuzi wa wanafunzi hao kwa lengo la kujiridhisha na sifa zao. Sifa zilizotakiwa ni ufaulu wa daraja la 1 hadi daraja la 3 na krediti mbili au zaidi katika masomo ya Sayansi na Hisabati,

“Lakini baada ya uchambuzi kufanyika kati ya wanafunzi wanaosomea ualimu wa sekondari 6,595 ni wanafunzi 382 pekee ndiyo wana sifa za kuendelea na masomo yao, 134 ni mwaka wa kwanza na 248 ni mwaka wa pili,” alisema Prof. Ndalichako.
 

Aidha alisema kuwa wengine 4,586 wa mwaka wa kwanza wa programu maalum wa stashahada ya ualimu wa sekondari waliokidhi vigezo vya ufaulu watahamishiwa katika vyuo vya ualimu vya serikali ambavyo ni Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu kuendelea na masomo na wanafunzi 1,337 wa mwaka wa pili watahamishiwa vyuo vya Korogwe na Kasulu ili kumalizia masomo yao.

Pia alisema kuwa serikali itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaoendelea kusoma UDOM na watarejea chuoni mwezi Oktoba mwaka huu, huku wale wa vyuo vya ualimu watakuwa wakilipiwa ada ya 600,000 kwa mwaka ambayo ndiyo ada ya vyuo hivyo na wataripoti chuoni mwezi Septemba.

Kwa upande wa wanafunzi wa kufundisha elimu ya shule ya msingi, Prof. Ndalichako alisema wanafunzi 29 wa mwaka wa pili ambao wana cheti cha daraja A la ualimu watahamishiwa Chuo cha Ualimu Kasulu ili wamalize masomo yao ila tu kwa gharama zao huku wengine 1,181 akiwataka waombe nafasi katika vyuo vingine katika masomo ambayo wana sifa zinazolingana nao.

Katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako alisema kuwa migomo iliyokuwa ikitokea chuoni UDOM kwa walimu kugoma kuwafundisha wanafunzi hao yawezekana ilikuwa ikichangiwa na wanafunzi hao kwani uwezo wa chuo cha UDOM ilikuwa ni kupokea wanafunzi 1,180 lakini wakapokea wanafunzi 7,805.

“Walimu kwao mzigo ulikuwa ni mzito wewe utafanya nini?, kwahiyo tukubali kuwa wingi wa wanafunzi ulichangia kutokea mgomo sababu walimu wameajiriwa kufundisha na wengine wa digrii sasa kupokea wanafunzi 7,805 na ilitakiwa 1,180 walikuwa wengi,” alisema Prof. Ndalichako.

  
Serikali imesema itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaorejeshwa UDOM na wanafunzi watakaohamishiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya Serikali watapewa mkopo wa kiasi cha Sh. 600,000/= kwa mwaka ambayo ni ada ya Mafunzo ya Ualimu itakayolipwa moja kwa moja Chuoni.

 May 28 2016 Serikali iliwarejesha nyumbani wanafunzi 7,805 waliokuwa wanasoma Stashahada Maalum ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati Chuo Kikuu Dodoma. Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na mgomo wa walimu uliokuwa umedumu kwa takribani wiki 3.

SOMA HAPA CHINI MCHANGANUO WA MAKUNDI HAYO MAALUM
  Kundi la Stashahada Maalumu ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari
Serikali imesema kwa kuwa uchambuzi umebainisha kuwa Wanafunzi wenye ufaulu wa Daraja la I na la II ambao pia wamefaulu masomo mawili ya Sayansi kwa kiwango cha C-A ni 382 (mwaka wa I -134 na mwaka wa II – 248), wanafunzi hao ndiyo pekee watakaorudishwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma ili wakamalizie mafunzo yao katika Chuo hicho.
Wanafunzi 4,586 wa mwaka wa I wa Programu Maalum ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari waliokidhi vigezo vya ufaulu watahamishiwa katika Vyuo vya Ualimu vya Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu kuendelea na masomo yao.
Wanafunzi 1,337 wa Mwaka II watahamishiwa kwenye Vyuo vya Ualimu vya Korogwe na Kasulu kumalizia masomo yao.
Wanafunzi 290 waliokuwa wamedahiliwa kusoma Programu Maalum ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari Masomo ya Sayansi na Hisabati ambao hawana sifa stahiki wanashauriwa kuomba mafunzo yanayolingana na sifa walizo nazo kwenye chuo chochote wanachotaka wao.
Kundi la Programu ya Ualimu wa Elimu ya Msingi
Serikali imesema wanafunzi katika kundi hili hawakuwa sehemu ya program maalum ya kupunguza uhaba wa walimu wa Sekondari wa Sayansi na Hisabati. Walikuwa wanaandaliwa kufundisha shule za msingi wakati lengo la Programu Maalum ilikuwa ni kukabiliana na tatizo za uhaba wa walimu wa Sekondari. Maudhui ya program waliyokuwa wanasoma hayakuwa sawasawa na yale ya Programu ya Ualimu wa Sekondari wa Sayansi na Hisabati.
Wanafunzi 29 wa mwaka wa II wenye Cheti cha Daraja IIIA waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Ualimu wa Shule za Msingi watahamishiwa katika Chuo cha Ualimu Kasulu wamalizie masomo yao kwa gharama zao wenyewe.
Wanafunzi 1,181 waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Kawaida ya Ualimu wa Elimu ya Msingi waombe mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo mahali popote watakapotaka wao.

No comments

+255716829257