Muhtasari: Habari kuu leo Alhamisi
1. UN: Marekani na Urusi ziokoe amani Syria
Mjumbe maalum wa Syria, Staffan De Mistura, ameziomba nchi mbili, Marekani na Urusi, kuzindua mikakati ya haraka ya kiwango cha juu, yenye nia ya kuokoa mazungumzo ya amani nchini Syria.
Baada ya kufahamisha baraza la usalama la Umoja wa mataifa, De Mistura amesema kuwa mpango wa kukomesha mapigano nchini humo, unayumbayumba na huenda ukasambaratika wakati wowote.
2. Watu 16 wauawa shambulio la Marekani Aleppo
Ripoti kutoka mji wa Aleppo nchini Syria, zinasema kwamba yamkini raia 16 wameuwawa katika shambulio la angani lililolenga hospitali moja na majumba yaliyokuwa karibu. Shambulio hilo lilitekelezwa na majeshi ya serikali. Watoto ni miongoni mwa waliouwawa.
3. Cruz ateua mgombea mwenza
Seneta wa Texas Ted Cruz, ambaye anatafuta nafasi ya kuteuliwa kukiwakilisha chama cha Republican kama Rais wake, katika uchaguzi mkuu wa Urais nchini Marekani amemtaja Carly Fiorina, afisa mkuu wa kampuni moja ya teknolojia kama mgombea mwenza.
Bi Fiorina alikuwa mwaniaji kiti cha urais kabla ya kujiondoa katika kinyanganyiro hicho, mwezi Februari.
4. Trump akosoa sera za Obama
Anayeongoza katika kinyang'anyiro cha kutaka kuteuliwa kugombea urais kupitia chama cha Republikan nchini Marekani, Donald Trump, ametoa hotuba yake ya kwanza inayohusu sera za mambo ya nje, ambapo ameishambulia vikali sera hiyo chini ya utawala wa Rais Barack Obama.
5. Waokoaji watafuta manusura Guatemala
Mamia ya waokoaji katika mji mkuu wa Guatemala, wanaendelea na msako wao kuwatafuta manusura waliofunikwa na taka, baada ya jaa la taka kuporomoka kutokana na mvua kubwa iliyonyesha.
Maiti nne zimeopolewa huku watu kadhaa wakinusuriwa, wakiwa hai. Wengi wao bado hawajulikani waliko.
6. Faida ya Facebook yaongezeka pakubwa
Na Kampuni ya mtandao wa kijamii ya Facebook imetangaza faida yake imeongezeka mara tatu katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka ikilinganishwa na kipindi sawa mwaka jana.
Kiwango hicho cha faida kilifikia dola bilioni 1 nukta tano. Wachanganuzi wanasema kuwa hiyo ni baada ya kuongezeka kwa mapato yatokanayo na matangazo katika simu tamba za smartphones.
7. Maandalizi ya kuunda serikali yaendelea Sudan Kusini
Maandalizi yanaendelea nchini Sudan Kusini ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, baada ya kurejea kwa kiongozi wa upinzani Dkt Riek Machar mjini Juba Jumanne ya wiki hii.
Aliapishwa kama makamu wa Rais kama sehemu ya muafaka wa amani wenye nia ya kukomesha mapigano ya kikabila ya muda mrefu, ambapo makumi kwa maelfu ya watu wameuwawa.
No comments
+255716829257