WANAOTUHUMIWA KUMVUA NGUO MTANZANIA, NCHINI INDIA WATIWA MBARONI.
Wanaume watano wanaotuhumiwa kuhusika katika kumshambulia na kumvua nguo mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 21 kutoka Tanzania wamekamatwa, shirika la habari la AP limeripoti.
Ubalozi wa Tanzania nchini humo umeitaka India kuhakikisha usalama wa wanafunzi wote kutoka Afrika wanaosomea nchini India, vyombo vya habari vinasema.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa India Sushma Swaraj, aliandika kwenye Twitter kwamba amesikitishwa sana na “kisa hicho cha aibu” kilichotokea Jumapili eneo la Bangalore.
Bi Swaraj amesema polisi wamewakamata washukiwa wanne ambao watafunguliwa mashtaka.
Kamishna wa polisi wa Bangalore N S Megharikh ameambia shirika la habari la AFP kwamba watu watano wamekamatwa kuhusiana na kisa hicho ambacho amesema kinaonekana kusababishwa na “hasira barabarani” na si “ubagusi wa rangi.”
"Tumewakamata watuhumiwa hao watano asubuhi baada ya kuwahoji usiku,” Megharikh ameambia AFP.
Mji wa Bangalore ni kitovu cha teknolojia ya habari na mawasiliano nchini India.
Wanafunzi Waafrika mjini Bangalore wamesema wanaishi na hofu ya kushambuliwa.
Bw Bosco Kaweesi, mshauri wa kisheria wa Chama cha Wanafunzi kutoka Afrika, anasema wanafunzi wengine watatu wa kike kutoka Tanzania waliokuwa pamoja na mwanafunzi huyo garini pia walipigwa.
Gari lao liliteketezwa.
Kaweesi amesema huenda kisa hicho kilitendeka kimakosa, akisema gari la wanafunzi hao lilikuwa limefuata gari la mwanafunzi kutoka Sudan ambalo lilimgonga na kumuua mwanamke mwenye umri wa miaka 35 aliyekuwa amelala pembezoni mwa barabara.
Wanafunzi hao hawakumfahamu mwanafunzi huyo wa kiume aliyetoka Sudan, ambaye pia alipigwa na gari lake kuteketezwa
No comments
+255716829257