Wakenya wagawanyika kuhusu ushindi wa Museveni
Muda mfupi baada ya Rais Yoweri Museveni kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Uganda, ujumbe wa Rais Uhuru Kenyatta akimpongeza kwa ushindi wake ulipakiwa kwenye kurasa zake Twitter na Facebook.
“Nina furaha sana kumpongeza Mtukufu Rais Yoweri Museveni kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Uganda. Watu wa Uganda wamenena, na wamenena kwa uwazi. Tunaheshimu uamuzi wao wa Rais Museveni.”
Rais Kenyatta alisema Kenya inathamini sana urafiki wa karibu ambao umekuwepo na kwamba anatarajia urafiki huo pamoja na ushirikiano hasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki utaendelea.
“Namtakia Rais Museveni ufanisi anapoendelea kutumikia taifa lake kwa muhula mwingine. Yeye na Uganda wanaweza kutarajia uungaji mkono wangu, na urafiki kutoka kwangu, pamoja na kutoka kwa kaka na dada zao hapa Kenya.”
Lakini hatua hiyo haikuwafurahisha baadhi ya Wakenya mtandaoni na wengi waliandika wakimshutumu.
Saa chache baadaye, kitambulisha mada#UhuruIsNotKenyakikaanza kuvuma kwenye Twitter. Kwenye Facebook, wengi waliandika kumkosoa.
Wakosoaji wake wanasema Rais Kenyatta alimpongeza Rais Museveni yeye binafsi na si kwa niaba yao.
Wengine walishangaa ni kwa nini Rais Kenyatta akaharakisha kumpongeza Rais Museveni ilihali “alichukua muda kumpongeza Dkt John Magufuli” alipotangazwa mshindi Tanzania”.
Lakini kunao wanaosisitiza kwamba Rais Kenyatta ana haki ya kumpongeza Rais Museveni bila "kuomba ushauri kutoka kwa wananchi".
Wengine wanaamini Rais Museveni anawakilisha "Afrika huru".
Rais Museveni amekuwa mmoja wa watu wanaopinga sana kesi zilizowasilishwa dhidi ya viongozi wakuu wa Kenya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Kesi dhidi ya Rais Kenyatta iliondolewa lakini kesi dhidi ya Naibu Rais William Ruto na mwanahabari Joshua arap Sang inaendelea.
Rais Museveni amehudhuria sherehe kadha za kitaifa na kupewa muda wa kuwahutubia wananchi.
No comments
+255716829257